• HABARI MPYA

    Friday, February 21, 2014

    NI WAKATI WA YANGA SC KUVUNJA MWIKO WA KUNYANYASWA NA WAARABU MICHUANO YA AFRIKA, AU HADITHI BADO NI ILE ILE?

    Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
    YANGA SC haijawahi kushinda mechi hata moja dhidi ya timu yoyote kutoka Kaskazini mwa Afrika, lakini mapema mwezi ujao watakuwa na mtihani mzito mbele ya mabingwa wa Afrika, Al Ahly ya Misri.
    Na kati ya timu za Kaskazini ambazo zimekuwa zikiinyanyasa Yanga SC, Al Ahly inaongoza zikiwa zimekutana mara sita na vigogo hao wa Misri wameshinda mechi nne na kutoa sare mbili.  
    ‘Bismillah’ Yanga inakutana kwa mara ya kwanza na Al Ahly na timu za Kaskazini kwa ujumla ilikuwa ni mwaka 1982 katika Raundi ya Pili ya Ligi ya Mabingwa na katika mchezo wa kwanza mjini Cairo, Waarabu hao walishinda 5-0 na marudiano Dar es Salaam timu hizo zikatoka sare ya 1-1.
    Wote wakali; Kutoka kulia Didier Kavumbangu, Simon Msuva na Mrisho Ngassa,wote hawa ni wachezaji tegemeo wa safu ya ushambuliaji Yanga SC
    Zikakutana tena mwaka 1988 katika Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa mchezo wa kwanza ukimalizika kwa sare ya bila kufungana Dar es Salaam wakati marudiano mjini Cairo, Yanga wakabebeshwa 4-0. 
    Mara ya mwisho Yanga kukutana na Ahly ilikuwa mwaka 2009 katika Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa pia na mchezo wa kwanza Cairo, wakafungwa 3-0 wakati marudiano Dar es Salaam wakafungwa pia 1-0.
    Vibonde wa Waarabu: Hawa ni baadhi ya wachezaji wa Yanga SC mwaka 2000, ambao walitolewa na Zamalek ya Misri katika Kombe la Washindi. Mstari wa mbele kutoka kulia Yahya Issa 'Gutta', Edibily Lunyamila, Chibe Chibindu na Abdulkadir Mohamed 'Tash'

    REKODI YA YANGA NA KASKAZINI AFRIKA:

    1982: RAUNDI YA PILI: (Ligi ya Mabingwa)
    Al- Ahly 5-0 Yanga SC (Cairo)
    Yanga SC 1-1 Al- Ahly (Dar es Salaam)
    1988: RAUNDI YA KWANZA: (Ligi ya Mabingwa)
    Yanga SC 0-0 Al-Ahly (Dar es Salaam)
    Al- Ahly 4-0 Yanga SC (Cairo) 
    1992: RAUNDI YA KWANZA: (Ligi ya Mabingwa)
    Yanga 0-2 Ismailia (Dar es Salaam)
    Ismailia 1-1 Yanga SC (Cairo)
    1998: KUNDI B: (Ligi ya Mabingwa)
    Raja Casablanca 6-0 Yanga SC (Casablanca) 
    Yanga SC 3-3 Raja Casablanca (Dar es Salaam)
    2007: RAUNDI YA PILI: (Ligi ya Mabingwa) 
    Esperance 3-0 Yanga SC (Tunis)
    Yanga SC 0-0 Esperance (Dar es Salaam)
    2009: RAUNDI YA KWANZA: (Ligi ya Mabingwa)
    Al Ahly 3-0 Yanga SC (Cairo)
    Yanga 0-1 Al Ahly (Dar es Salaam)
    2000: RAUNDI YA KWANZA: Kombe la Washindi
    Yanga 1-1 Zamalek (Misri)
    Zamalek 4-0 Yanga SC (Cairo)
    2008: RAUNDI YA KWANZA: Kombe la Shirikisho 
    Al-Akhdar (Libya) 1-1 Yanga SC (Tripoli) 
    Yanga SC 0-1 Al-Akhdar (Dar es Salaam)
    Machi 1, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga SC watajaribu kupata ushindi wa kwanza kabisa dhidi ya Ahly na timu za Kaskazini kwa ujumla katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Kwanza Ligi ya Mabingwa Afrika, au Hatua ya 16 Bora.
    Na Machi 8 Uwanja wa Kimataifa wa Cairo, Misri Yanga watajaribu kuitoa mashindanoni kwa mara ya kwanza kabisa timu ya Kaskazini mwa Afrika tangu ianze kukutana nazo 1982.
    Yanga SC mwaka huu inaonyesha kudhamiria kuvunja mwiko wa kunyanyaswa na Ahly na timu za Kaskazini mwa Afrika kwa ujumla- kutokana na aina ya maandalizi yake.
    Mapema Januari ilikwenda kuweka kambi ya karibu wiki mbili mjini Antalya, Uturuki na pamoja na mazoezi makali, ilipata mechi nne za kujipima nguvu dhidi ya timu za Ulaya na kushinda mbili na kutoa sare mbili.
    Ikumbukwe Desemba mwaka jana Yanga SC ilivunja benchi lake zima la Ufundi, ikiwaondoa Kocha Mkuu Mholanzi, Ernie Brandts na Wasaidizi wake Freddy Felix Minziro na Razack Ssiwa na kuwaajiri Mholanzi mwingine, Hans van der Pluijm na Wasaidizi wake, Charles Boniface Mkwasa na Juma Pondamali.
    Ilibadilisha hadi Daktari wa timu,  ikmpiga chini Nassor Matuzya na kumuajiri Juma Sufiani.  
    Tangu imerejea kutoka Uturuki, Yanga SC haijapoteza mechi hata moja katika Ligi Kuu ikishinda mbili nyumbani na kutoka sare moja ugenini, wakati katika Ligi ya Mabingwa, iliitoa Komorozine ya Comoro kwa jumla ya mabao 12-0, ikishinda 7-0 nyumbani na 5-2 ugenini.
    Hii inaashiria kwamba Yanga SC ya mwaka huu ni tofauti kidogo na Yanga zile ambazo Al Ahly imezoea kukutana nazo miaka ya nyuma.
    Al Ahly ilileta wawakilishi wake mwezi huu kuja kuitazama Yanga ikimenyana na Komorozine Dar es Salaam na mabingwa hao wa Bara nao wakampeleka kocha wao Msaidizi, Charles Boniface  Mkwasa kwenda kuwatazama Waarabu hao wakimenyana na CS Sfaxien ya Tunisia jana katika mechi ya Super Cup mjini Cairo.
    Amr Gamal ndiye tegemeo la mabao la Al Ahly hivi sasa 
    Yanga SC imekuwa kambini Bagamoyo tangu imerejea kutoka Uturuki, na imekuwa ikitokea huko kwenda kwenye mechi zake zote na kurejea huko huko.
    Na kesho watatokea huko kwenda Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kumenyana na Ruvu Shooting katika mchezo wa Ligi Kuu, ambao utakuwa wa mwisho kabla ya kuvaana na Waarabu wa Misri.
    Inaonekana ni kiasi gani Yanga SC chini ya Mwenyekiti wake, Bilionea Yussuf Manji imedhamiria kufanya mapinduzi. 
    Kiasi cha Sh. Milioni 200 kimekusanywa chini ya Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Kimataifa ya Yanga SC, Seif Ahmed ‘Magari’ kwa ajili ya motisha kwa wachezaji wacheze kwa bidii washinde.
    Usiwasahau na hawa; Kutoka kulia kipa Juma Kaseja na washambuliaji hatari wa Yanga SC, Waganda, Emmanuel Okwi na Hamisi Kiiza 
    Ushindi wa mabao 3-0 mjini Dar es Salaam utafanya wachezaji hao wagawiwe Sh. Milioni 200 zote, wakishinda mabao 2-0 watapewa Sh. Milioni 100 wagawane na wakishinda bao 1-0 watapewa Sh. Milioni 50.
    Kama watashinda chini ya mabao 3-0 kiasi cha fedha kitakachobaki kitawekwa na watapewa chote iwapo watamalizia vizuri mchezo wa marudiano Cairo na kufuzu. 
    Je, Yanga SC itavunja mwiko wa kunyanyaswa na Al Ahly na timu za Kaskazini kwa ujumla? Bila shaka hilo ni jambo la kusubiri na kuona.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NI WAKATI WA YANGA SC KUVUNJA MWIKO WA KUNYANYASWA NA WAARABU MICHUANO YA AFRIKA, AU HADITHI BADO NI ILE ILE? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top