• HABARI MPYA

    Friday, February 21, 2014

    TFF YAPANGUA TENA RATIBA LIGI KUU, MECHI YA AZAM NA PRISONS YASUKUMWA MBELE

    Na Boniphace Wambura, Dar es Salaam
    LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inaingia Raundi ya 19 kesho (Februari 22 mwaka huu) kwa mechi tano zitakazochezwa katika miji ya Dar es Salaam, Bukoba, Morogoro, Tanga na Arusha.
    Yanga itakuwa mgeni wa Ruvu Shooting ya mkoani Pwani katika mechi itakayofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Nayo Kagera Sugar inaikaribisha Rhino Rangers ya Tabora katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
    Mechi kati ya Azam FC na Prisons iliyokuwa ichezwe kesho imesogezwa mbele hadi Jumapili

    Uwanja wa Manungu uliopo Turiani mkoani Morogoro ndiyo utakaotumika kwa mechi kati ya Mtibwa Sugar na Ashanti United, wakati Coastal Union itaumana na Mbeya City katika mechi itakayooneshwa moja kwa moja na Azam Tv kutoka Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga. Maafande wa Oljoro JKT watakuwa nyumbani kupambana na Mgambo Shooting katika mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha.
    Jumapili (Februari 23 mwaka huu) katika Uwanja wa Taifa ni Simba dhidi ya JKT Ruvu, mechi ambayo pia itaoneshwa moja kwa moja na Azam Tv. 
    Mechi kati ya Azam na Tanzania Prisons iliyokuwa ichezwe kesho (Februari 22 mwaka huu) Uwanja wa Chamazi sasa itachezwa Jumapili (Februari 23 mwaka huu) ambapo na itakuwa ‘live’.
    Ligi hiyo itaendelea Jumatano (Februari 26 mwaka huu) kwa mechi moja kati ya Ashanti United na Azam itakayochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex (Chamazi).
    Wakati huo huo:  Michuano ya mikoa katika mpango maalumu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuboresha Taifa Stars inaanza kutimua vumbi kesho (Februari 22 mwaka huu) kwa mechi nne.
    Mechi rasmi ya ufunguzi wa michuano hiyo inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itakuwa kati ya Ilala na Temeke. Mechi hiyo ya kundi G itachezwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume kuanzia saa 9.30 alasiri.
    Kundi A kutakuwa na mechi kati ya Pwani na Morogoro kwenye Uwanja wa Mabatini mjini Mlandizi wakati Kusini Unguja na Kaskazini Unguja zitacheza kwenye Uwanja wa Mao Tse Tung mjini Unguja katika kundi H.
    Kusini Pemba na Kaskazini Pemba zitacheza mechi ya Kundi I katika Uwanja wa Gombani kisiwani Pemba.
    Mechi za keshokutwa (Februari 23 mwaka huu) ni Simiyu itacheza na Shinyanga mjini Bariadi katika kundi E. Nayo Ruvuma itacheza na Njombe kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea katika kundi D.
    Kundi C ni Tanga na Kilimanjaro kwenye Uwanja wa Mkwakwani wakati Kagera itacheza na Geita kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba katika kundi B. Mtwara itacheza na Lindi kwenye Uwanja wa Nangwanda mjini Mtwara katika kundi F.
    Wang’amuzi 40 wa vipaji tayari wamesharipoti kwenye vituo vya mechi hizo kwa ajili ya kufanya kazi hiyo.

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TFF YAPANGUA TENA RATIBA LIGI KUU, MECHI YA AZAM NA PRISONS YASUKUMWA MBELE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top