• HABARI MPYA

    Tuesday, February 18, 2014

    ZENGWE LINGINE LA OKWI LATUA TFF

    Na Boniface Wambura, Dar es Salaam
    SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limewalalamikia wana familia watano wa mpira wa miguu kwa Kamati ya Maadili kuhusiana na udanganyifu katika mtihani wa utimamu wa mwili wa waamuzi na usajili wa mchezaji Emmanuel Okwi.
    Riziki Majala na Army Sentimea ambao ni wakufunzi wa waamuzi, na Oden Mbaga na Samwel Mpenzu ambao ni waamuzi wanadaiwa kughushi nyaraka kuhalalisha mtihani huo kinyume cha taratibu.
    Emmanuel Okwi kushoto akiichezea Etoile du Sahel ya Tunisia

    Naye Sabri Mtulla analalamikiwa na TFF kwa madai ya kuidanganya Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji kuwa hakukuwa na pingamizi lolote juu ya usajili wa mchezaji Emmanuel Okwi huku akijua wazi kuwa jambo hilo si kweli.
    Kwa mujibu wa kanuni, malalamiko hayo yamefikishwa kwenye Kamati ya Maadili ambayo itachunguza ili kujiridhisha kama yana msingi au la. Ikibaini kuna kesi ndipo walalamikiwa watafika mbele ya kamati hiyo.
    Wakati huo huo: Stand United ya Shinyanga imekata rufani TFF ikipinga Kanembwa JKT ya Kigoma kuchezesha wachezaji waliosajiliwa katika dirisha dogo kwenye mechi ya kiporo iliyozikutanisha timu hizo.
    Mechi hiyo namba 22 ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ilichezwa juzi (Februari 16 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora ambapo Kanembwa JKT iliibuka na ushindi wa bao 1-0.
    Katika rufani yake, Stand United inadai kwenye mechi hiyo Kanembwa JKT ilichezesha wachezaji wanane waliosajiliwa katika dirisha kidogo kinyume na maelekezo kutoka TFF kwa timu hizo kuwa wachezaji waliosajiliwa katika dirisha dogo hawawezi kucheza mechi hiyo.
    Wachezaji wanaodaiwa kusajiliwa dirisha dogo na kucheza mechi hiyo ni Hamidu Juma, Ibrahim Shaban Issa, Joseph Mlary, Lucas Charles Karanga, Raji Ismail, Salvatory Kulia Raphael, Seif Ibrahim Zaid na Yonathan David Sabugowiga.
    Dirisha dogo lilifunguliwa Novemba 15 na kufungwa Desemba 15 mwaka jana, hivyo Stand United katika rufani yake inaombwa ipewe pointi tatu na mabao matatu kwa Kanembwa JKT kuchezesha wachezaji wasiostahili.
    Awali mechi hiyo ilichezwa Novemba 2 mwaka jana Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, na kuvunjwa na mwamuzi dakika ya 87 baada ya Kanembwa JKT kugomea pigo la penalti dhidi yao.

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ZENGWE LINGINE LA OKWI LATUA TFF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top