• HABARI MPYA

    Wednesday, February 19, 2014

    RUVU SHOOTING WATUMA SALAMU YANGA; “TUTAWATIA NGWALA JUMAMOSI”

    Na Princess Asia, Dar es Salaam
    RUVU Shooting wametuma salamu Yanga SC, kuelekea mchezo wa Jumamosi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara wakiwaambia kwamba watawatia doa siku hiyo. 
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY jioni hii, Msemaji wa Ruvu, Massau Bwire amesema kwamba anafahamu Yanga wameshika kasi kwenye kwenye mbio za ubingwa, lakini Jumamosi watawatia ngwala.
    “Tumejipanga vzuri mno kuelekea mchezo huo na tumedhamiria kweli kushinda, kwa kweli tunahitaji kuonyesha tuna uwezo kwa kiasi gani,”alisema Bwire.
    Kikosi cha Ruvu Shooting, wa kwanza kushoto waliosimama Hassan Dilunga amehamia Yanga SC dirisha dogo pamoja na kocha Charles Boniface Mkwasa  

    Lakini Kocha Msaidizi wa Yanga SC, Charles Boniface Mkwasa alikuwa kocha wa Ruvu Shooting kwa misimu zaidi ya mitatu hadi Desemba mwaka jana alipohamia Yanga, hivyo anaifahamu vizuri timu hiyo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
    Kuhusu hilo, Bwire anasema; “Mkwasa kutujua sisi si tija, tumepata kocha mpya (Mkenya Thom Olaba) ambaye ni mzuri na katika yale ambayo aliyaacha hapa Mkwasa, huyu kocha wetu mpya amebadilisha mambo kwa kiasi kikubwa. Kwa ujumla ameibadilisha timu sana,”.
    Charles Boniface Mkwasa kushoto alikuwa kocha wa Ruvu Shooting hadi Desemba alipohamia Yanga SC

    “Tarajia kuiona Ruvu Shooting tofauti na ile uliyokuwa unaiona wakati wa Mkwasa. Tumemnyoa mzee wa Oman, na sasa tunataka kumnyoa mzee wa Uturuki,”alisema Bwire akimaanisha baada ya kuifunga 1-0 Coastal Union Jumamosi ambayo iliweka kambi Oman mwezi uliopita, sasa watawafunga Yanga walioweka kambi Uturuki mwezi huo huo.
    Yanga SC inafukuzana na Azam FC na Mbeya City katika mbio za ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu, ingawa pia na Simba SC hawapo mbali sana.
    Yanga SC ina pointi 35 baada ya kucheza mechi 16 sawa na Mbeya City iliyocheza mechi 18, wakati Azam FC yenye pointi 36 baada ya kucheza mechi 16, ipo kileleni mwa ligi hiyo. Simba SC yenye pointi 32 baada ya kucheza mechi 18, ipo nafasi ya nne.
    Mechi nyingine za mwishoni mwa wiki ni kati ya Kagera Sugar na Rhino Rangers Uwanja wa Kaitaba Bukoba, Mtibwa Sugar na Ashanti United Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro, Coastal Union na 
    Mbeya City Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, JKT Oljoro FC na JKT Mgambo Uwanja wa Sheikh Ameri Abeid, Arusha na Azam FC na Prisons Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: RUVU SHOOTING WATUMA SALAMU YANGA; “TUTAWATIA NGWALA JUMAMOSI” Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top