![]() |
| Rais wa TFF, Leodegar Tenga |
Na Boniface Wambura
KAMATI ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) inakutana Mei 9, mwaka huu jijini Dar es Salaam kupokea na kupanga utekelezaji wa maagizo ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kuhusu uchaguzi wa shirikisho hilo la nchi.
Kikao hicho cha dharura chini ya Uenyekiti wa Rais wa TFF, Leodegar Tenga kitakuwa na ajenda hiyo moja tu katika kuhakikisha utekelezaji wa maelekezo ya FIFA unafanyika haraka ili uchaguzi ufanyike ndani ya muda uliopangwa.
FIFA katika maelekezo yake imetaka kwanza ziundwe Kamati ya Maadili na Kamati ya Rufani ya Maadili kabla ya kuingia kwenye mchakato wa uchaguzi wa Kamati mpya ya Utendaji ya TFF. FIFA imeagiza uchaguzi uwe umefanyika kabla ya Oktoba 30 mwaka huu.
Katika hatua nyingine, Kamati ya Mashindano ya TFF inakutana Jumapili (Mei 5 mwaka huu) kupitia maandalizi ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) iliyopangwa kuanza Mei 12 mwaka huu.
Tayari mikoa 18 kati ya 27 kimpira imeshapata mabingwa wao kwa ajili ya RCL itakayotoa timu tatu zitakazopanda daraja kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu ujao (2013/2014).
Kamati hiyo chini ya Uenyekiti wa Blassy Kiondo ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF itapokea taarifa ya maandalizi ya ligi hiyo kutoka Idara ya Mashindano ya TFF na kufanya uamuzi juu ya mikoa ambayo haijawasilisha mabingwa wao.
Ligi hiyo itachezwa kwa mtindo wa nyumbani na ugenini, na ratiba (draw) itapangwa wakati wowote. Ada ya kushiriki ligi hiyo kwa kila klabu ni sh. 100,000 na usajili utakaotumika na ule ule wa ligi ngazi ya mkoa. Hakutakuwa na usajili mpya wa wachezaji.



.png)