• HABARI MPYA

    Monday, May 27, 2013

    YANGA SC WAISAIDIA SIMBA SC KUSAFISHA JINA NA KUREJESHA HADHI

    Kiberenge cha Msimbazi; Haruna Chanongo wa Simba kushoto akimtoka David Luhende wa Yanga Mei 18, mwaka huu. Simba ililala 2-0. Kijana ameongeza mkataba Simba SC.

    Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA MEI 27, 2013 SAA 4:30 ASUBUHI
    SIMBA SC imeonyesha nidhamu ya hali ya juu ya matumizi ya fedha, baada ya kutumia fedha ilizopata kutokana na mapato ya mechi dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga SC Mei 18, mwaka huu kusajili wachezaji wapya wane na kuwaongeza mikataba wengine, zaidi ya watatu sambamba na kulipa madeni yaliyokuwa yanawakanili katika hoteli za Spice na Sapphire, Kariakoo, Dar es Salaam.
    Simba SC ilipata mgawo wa Sh. 123,970,927.45 kutokana na mapato ya Sh. 500,390,000 ya mechi hiyo waliyofungwa 2-0 na tayari imefuta deni la Sh. Milioni 27 ilizokuwa inadaiwa na hoteli ya Spice kiasi cha kukamatwa kwa gari zao mbili, basi dogo na salon na pia imelipa sehemu kubwa ya deni la Sapphire.
    Kana kwamba hiyo haitoshi, Simba SC imetumia fedha hizo kusajili wachezaji wapya wanne, kipa Andrew Ntala kutoka Kagera Sugar, beki Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ kutoka Mtibwa Sugar, kiungo Twaha Shekuwe ‘Messi’ kutoka Coastal Union na mshambuliaji Zahor Pazi kutoka Azam FC, aliyekuwa anacheza kwa mkopo JKT Ruvu.
    Simba SC imewaongezea mikataba wachezaji wake chipukizi kadhaa iliyowapandisha kutoka kikosi cha pili akiwemo Haruna Chanongo, ambaye alikuwa anapigiwa hesabu na wapinzani wao wa jadi, Yanga SC.
    Baada ya kufanya mambo hayo makubwa, Simba sasa itafungua akaunti yake kutoa fungu la bajeti ya usajili wa wachezaji wawili wa kigeni, beki wa kati na mshambuliaji sambamba na kusaini mikataba mipya na Nahodha wake Juma Kaseja pamoja na kiungo Amri Kiemba.
    BIN ZUBEIRY inafahamu Simba SC imekwishafanya mazungumzo na wachezaji wawili wa kigeni, wanaochezea timu zao za taifa na muda si mrefu itawataja baada ya kukamilisha usajili wao.
    Simba SC inafanya usajili wake kwa tahadhari, kwa kuhofia Yanga SC wasiwatibulie kama walivyofanya kwa Mbuyu Twite msimu uliopita.
    Mechi dhidi ya Yanga, ya kuhitimisha Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2012/2013 ilishuhudiwa na watazamaji 57,406 waliokata tiketi kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 7,000, sh. 10,000, sh. 15,000, sh. 20,000 na sh. 30,000.
    Kila klabu ilipata mgawo wa Sh. 123,970,927.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 76,330,677.97.
    Kiingilio cha sh. 5,000 ndicho kilichovutia watazamaji wengi ambapo waliokata tiketi hizo walikuwa 19,039 na kuingiza sh. 95,195,000 wakati kile cha sh. 7,000 kiliingiza watazamaji 17,647 na kupatikana sh. 123,515,000.
    Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 63,036,064.81, tiketi sh. 3,818,890, gharama za mechi sh. 37,821,638.88, Kamati ya Ligi sh. 37,821,638.88, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 18,910,819.44 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 14,708,415.12.
    Kwa kulipa madeni hayo, Simba SC sasa imejisafisha na kurejesha hadhi yake, kwani ilikwishaanza kupotea kutokana na kulimbikiza madeni.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: YANGA SC WAISAIDIA SIMBA SC KUSAFISHA JINA NA KUREJESHA HADHI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top