• HABARI MPYA

    Sunday, May 26, 2013

    RAIS KIKWETE AMEWAPA CHANGAMOTO NZURI TFF, WAIFANYIE KAZI


    IMEWEKWA MEI 26, 2013 SAA 12:30 ASUBUHI
    ALHAMISI wiki hii, RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete aliwaalika Ikulu wachezaji wa timu ya soka ya taifa, Taifa Stars na akazungumza nao mambo kadhaa, kubwa kuwahamasisha katika kampeni yao ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia, mwakani nchini Brazil.
    Ikumbukwe, hadi sasa, Stars inashika nafasi ya pili katika Kundi C, ikiwa na pointi sita baada ya kucheza mechi tatu kushinda mbili na kufungwa moja, nyuma ya Ivory Coast yenye pointi saba, iliyoshinda mechi mbili na kutoa sare moja.

    Kama Stars itashinda mechi yake ijayo ugenini dhidi ya Morocco, Juni 8, mwaka huu itajiweka katika nafasi nzuri ya kuingia kwenye hatua ya mwisho ya kuwania tiketi ya Brazil.
    Ikifanikiwa kumaliza kileleni kwa Kundi hilo, lenye timu za Ivory Coast, Morocco na Gambia pia, Stars itacheza mechi mbili za mwisho nyumbani na ugenini dhidi ya moja ya timu zitakazoongoza makundi  na ikishinda itaweka historia ya kucheza Fainali za Kwanza za Kombe la Dunia.
    Stars, imekuwa na mwenendo mzuri chini ya Mdenmark Kim Pouslen, ambaye ameiwezesha kushinda mechi tano kati ya 10, sare tatu na kufungwa mbili tangu aanze kazi Mei mwaka jana, akirithi mikoba ya Mdenmark mwenzake, Jan Poulsen.
    Hakika mwenendo huo umemvutia Rais Kikwete na wiki hii akaona vema akutane na vijana kabla hawajaenda Morocco kucheza mechi yao ya kwanza ya mzunguko wa pili. Mheshimiwa Rais alisema mengi kiasi fulani, akiwaahidi wachezaji wa timu hiyo kuwafanyia kitu kizuri ambacho kitakuwa kumbukumbu nzuri katika maisha yao, iwapo wataongoza Kundi C. 
    Lakini pamoja na hayo, Rais Kikwete alizungumzia mustakabali mzima wa timu hiyo na akalitaka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kujenga uwezo wa kuwalipa makocha wa Taifa Stars, ili Serikali inayotekeleza jukumu hilo kwa sasa, ifikie wakati ijivue mzigo huo.
    Alisema kwamba Serikali imelazimika kuendelea kulipa mishahara ya makocha wa timu ya taifa, kwa sababu bado TFF hawana uwezo wa kufanya hivyo.
    Hata hivyo, Rais Kikwete alimtaka Rais wa TFF, Leodegar Chillah Tenga kuhakikisha wanajenga uwezo wa kulipa maocha wa timu hiyo na kuipunguzia mzigo huo Serikali.
    Rais Kikwete alianza kugharamia mishahara ya makocha tangu alipoingia Ikulu mwaka 2005 na mwalimu wa kwanza alikuwa ni Mbrazil Marcio Maximo aliyeanza kazi Juni mwaka 2006 nchini, akafuatiwa na Mdenmark, Jan Borge Poulsen mwaka 2010 na sasa Mdenmark mwingine, Kim Poulsen aliyeanza kazi Mei mwaka jana.
    Kwa kweli wapenzi wa soka nchini wana kila sababu ya kumshukuru Rais Kikwete, kwa kazi kubwa aliyoifanya katika kujenga ustawi mpya wa timu ya taifa, kwani hali ilikwishakuwa mbaya na timu hiyo ilipoteza mvuto na hadhi yake, kaisi hata cha wachezaji kutokuwa na hamu nayo.
    Lakini leo kila mchezaji anataka kuchezea timu ya taifa na hata klabu zinapenda kuona wachezaji wao wanaitwa Taifa Stars. Hii imetokana na juhudi za dhati za Rais Kikwete tangu ameingia Ikulu mwaka 2005, kujitolea kusaidia kwa hali na mali ustawi mpya wa timu hiyo.
    Leo Taifa Stars ina ufadhili mnono wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia ya Kilimanjaro, inashiriki mashindano kwa uhakika na ndiyo maana hata nguvu ya kupambana kwa ajili ya nafasi inapatikana.
    Lakini pamoja na ukweli huo wa msaada wa Rais, hatupaswi kusahau kwamba soka ni mchezo ambao unasimamiwa na taasisi maalum na hiyo si nyingine, bali TFF. Lazima ufike wakati, taasisi hiyo kama ilivyojipa mamlaka kamili ya kusimamia mambo yake, bila kuingiliwa hata na dola, basi iweze kujimudu kwa kila hali.
    Umefika wakati tuone faida ya kuwa na viongozi wasomi katika soka yetu kwa kuonyesha weledi na ubunifu wao, kwa kuifanya soka ya Tanzania iweze kujidumu kupitia taasisi yake na kuepuka kutegemea misaada.
    Suala kama mshahara wa kocha, kama TFF iliingia Mkataba wa udhamini na TBL, je haikujua kwamba timu itahitaji kuwa na kocha, ambaye atahitaji bajeti maaalum ya kuwepo kwake nchini kufanya kazi? Na mbona mishahara ya makocha inaendelea kuwa mzigo wa Serikali?
    Watu hawawezi kupinga Serikali kusaidia michezo, lakini kuna maeneo mengi ambayo Serikali inahitajika, tena kwa dhati kutia mkono wake, lakini si kwa timu ya taifa ambayo kwa sasa inaonekana kabisa kuogelea kwenye bwawa la udhamini mnono wa TBL.
    Pamoja na yote, suala la makocha, nchi nyingi hapa hapa kwetu Afrika, tena ukanda huu huu wa CECAFA, makocha wanalipwa na vyama vya soka vya nchi husika- kwa nini TFF inashindwa kufanya hivyo?
    Tuache kuishi kwa mazoea, kwamba eti hata wakati Mwalimu Julius Nyerere makocha wa Stars walikuwa walikuwa wanalipwa na Serikali- hapana, lazima tukubali kubadilika kwa ujumla. 
    Rais JK amewapa changamoto nzuri TFF, waifanyie kazi. Umefika wakati wajenge uwezo wa kujidumu kikamilifu. Jumapili njema.     
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: RAIS KIKWETE AMEWAPA CHANGAMOTO NZURI TFF, WAIFANYIE KAZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top