• HABARI MPYA

    Tuesday, May 28, 2013

    MAN NGWAIR AFARIKI DUNIA AFRIKA KUSINI LEO

    RIP; Ngwair
    Na Mwandishi Wetu, IMEWEKWA MEI 28, 2013 SAA 12:00 JIONI

    MSANII maarufu wa Bongo Fleva, Albert Mangwea maarufu kama Ngwair, amefariki dunia leo akiwa nchini Afrika Kusini.
    Kwa mujibu wa taarifa za Redio mbalimbali jioni hii nchini, inadaiwa Ngwair amefariki dunia kutokana na matatizo ya matumizi ya dawa za kulevya. 
    Kimuziki, Ngwair aliibukia kwenye Dodoma ambako alikuwa katika kundi moja na Noorah na Mez B.
    Baadaye akapata dili Bongo Records chini ya mmiliki wa studio hizo, Petter Matthysse ‘P Funk’ aliyemuinua zaidi kimuziki na kumfanya awe miongoni mwa wanamuziki nyota nchini.
    Wimbo wake wa kwanza kutamba ni Gheto Langu mwaka 2003 ambao ulimpatia umaarufu kabla ya kutoa albamu yake ya kwanza a.k.a Mimi mwaka 2003 ambayo ilimpatia mafanikio makubwa na kubadili maisha yake.
    Hata hivyo, mafanikio hayo yalimlevya na kujitumbukiza kwenye utumiaji wa dawa za kulevya, hivyo kujikuta akishindwa kufanya kazi ya muziki kwa usanifu na kuanza taratibu kufilisika hadi kuuza mali zake zote, ikiwemo gari aina ya Jeep.
    Ngwair kutoka kwenye kupanga nyumba nzima maeneo ya Sinza, Dar es Salaam akajikuta anarejea kuishi katika ‘magheto’ ya washkaji zake sehemu mbalimbali Dar es Salaam.
    Mwaka 2010, Athumani Tippo, mmiliki wa maduka ya Zizzou Fashions alijaribu kumuinua tena msanii huyo baada ya kumchukua kwenye lebo yake na kumuwezesha kutoa albamu ya pili, Nge.
    Hata hivyo, Nge haikufanya vizuri sana na kuzidi kumchanganya msanii huyo hivyo kutopea kwenye dimbwi la utumiaji wa dawa za kulevya na ‘kuharibika zaidi’.  
    Mafanikio yake zaidi ni kushinda tuzo ya Kilimanjaro Music Awards kama mwana Hip Hop Bora wa mwaka 2005. 
    Mwaka 2003, msanii Wayne Wonder aliyekuja kutumbuiza kwenye Fiesta aliondoka na CD ya wimbo Mikasi ya Ngwair baada ya kuvutiwa na kibao hicho alichowashirikisha Mchizi Mox na Ferooz. Pumzika kwa amani. Mbele yako, nyuma yetu Ngwair. RIP.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: MAN NGWAIR AFARIKI DUNIA AFRIKA KUSINI LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top