• HABARI MPYA

    Thursday, May 02, 2013

    HAACHWI HATA MCHEAJI MMOJA YANGA MSIMU UJAO

    Haachwi mtu; Wachezaji wa Yanga wakishangilia ushindi katika moja ya mechi zao, habari zinasema hataachwa yeyote kati yao

    Na Prince Akbar
    KWA mara ya kwanza baada ya muda mrefu, msimu huu Yanga SC huenda isiache mchezaji hata mmoja kutoka kikosi chake kilichoipa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Habari kutoka ndani ya Yanga, ambazo BIN ZUBEIRY imezipata zimesema kwamba, klabu imeridhishwa na uwajibikaji wa wachezaji wote kikosini, wakiwemo wale ambao hawana namba kwenye kikosi cha kwanza.
    Habari zimesema kwamba, wachezaji ambao hawachezi kwenye kikosi cha kwanza ripoti zao za mazoezini ni nzuri, hivyo wataendelea kupewa muda kwa msimu mwingine.
    “Labda klabu inaweza kumruhusu mchezaji kuondoka. Kama ameona hapati nafasi na yeye amejikatia tamaa, na mwalimu akatuambia tunaweza kumruhusu, tutamruhusu,”alisema kigogo mmoja wa mambo ya usajili Yanga SC.
    Hata hivyo, kigogo huyo alisema kwamba Yanga inaweza kuuza wachezaji ambao watatakiwa na timu nyingine za ndani au nje, iwapo itaridhika na ofa zitakazotolewa.
    “Zikija ofa nzuri, tutauza mchezaji. Iwe klabu ya hapa au ya nje. Sisi ni klabu ambayo sasa tunataka kujiendesha kibiashara. Atakayeleta ofa nzuri kwa mchezaji wetu yeyote, tukaridhia, tutamuuzia,”alisema.
    Lakini kigogo huyo, alisema kwamba mpango wa kusajili wachezaji wachache tu kuongeza nguvu kikosini upo na kwamba zoezi hilo litafanyika kwa umakini wa hali ya juu.
    “Tunajua tunakwenda kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Na tumeuona uwezo wa timu yetu unaishia wapi. Hivyo tutahitaji wachezaji kama watatu wa kuongeza nguvu katika idara fulani fulani,”.
    “Kati yao, mmoja lazima awe mshambuliaji wa kigeni. Hapa ndipo sehemu ambayo Yanga itatuliza sana akili. Tunataka mchezaji ambaye akija hapa atakuwa mshambuliaji kweli. Awe na uwezo mkubwa kuliko washambuliaji wote Tanzania,”alisema.
    Baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu kwa mara ya 24 tangu walipotwaa mara ya kwanza mwaka 1968, Yanga SC sasa wanajiandaa kufunga msimu kwa mpambano dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Simba SC Mei 18, mwaka huu.     
    Siku hiyo, ndipo kutakuwa na sherehe ya mabingwa hao kukabidhiwa Kombe lao na Yanga SC imepania kukabidhiwa taji kwa mashamsham kwa kuhakikisha wanawafunga wapinzani wao hao wa jadi.
    Na Yanga imepania kulipa kisasi cha mabao 5-0 waliyofungwa na Simba SC msimu uliopita katika Ligi Kuu. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: HAACHWI HATA MCHEAJI MMOJA YANGA MSIMU UJAO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top