• HABARI MPYA

    Thursday, February 13, 2020

    VANDENBROECK APEWA ONYO, AYMAEL, MANARA NA NUGZA WAPELEKWA KAMATI YA NIDHAMU TFF

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KOCHA wa Simba SC, Steven Ludwig Vandenbroeck amepewa onyo kali kwa kosa la kugoma kuwafungulia mlango mwamuzi na Kamishina wakati wa mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Coastal Union ya Tanga Februari 1, mwaka huu Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.
    Taarifa ya Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kwa Vyombo vya Habari leo imesema kwamba adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni namba 41(13) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti wa Makocha.
    Taarifa imeongeza kwamba maamuzi hayo yamefikiwa katika kikao cha Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi kilichokaa Februari 10, mwaka huu.
    Naye refa msaidizi namba mbili, Kassim Mpanga amefungiwa miezi mitatu kwa kosa la kushindwa kutafsiri sheria za mpira wa miguu katika mechi kati ya Simba SC na JKT Tanzania Februari 7 Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni namba 39(1) ya Ligi Kuu Kuhusu Udhibiti wa Waamuzi.
    Aidha, Kikao cha Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi kilichokaa Jumatatu, kimeielekeza Sekretarieti kufuatilia viongozi wa vilabu na Makocha ambao hivi karibuni wamekuwa wakishutumu na kutoa matamshi yenye kukashifu na kudhalilisha viongozi ,Chapa (Brand) ya Ligi na Taasisi kwa ujumla kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kwa vipindi tofauti tofauti.
    Viongozi na Makocha waliobainika ni wafuatao Kocha wa Klabu ya Namungo FC(Hitimana )-kwenye mchezo wa Simba SC na Namungo Fc, Kocha wa Klabu ya Young African Sc (Luc Aymael)-kwenye mchezo wa Yanga Sc na Lipuli, Msemaji wa Klabu ya Simba SC (Haji Manara) na Muhamasishaji wa Young African sc(Anthonio Nugaz) .
    Kutokana na matamshi hayo wanapelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: VANDENBROECK APEWA ONYO, AYMAEL, MANARA NA NUGZA WAPELEKWA KAMATI YA NIDHAMU TFF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top