• HABARI MPYA

    Monday, February 17, 2014

    TUZO ZA KILI 2014 ZAZINDULIWA LEO DAR, WAKALI KUJIBEBEA VYAO MEI 3 MLIMANI CITY

    Na Renatus Mahima, Dar es Salaam
    TUZO kwa wanamuziki waliofanya vizuri nchini mwaka huu (Kilimanjaro Tanzania Music Awards 2014) zimezinduliwa leo mchana na kilele chake kitakuwa Mei 3 katika hafla kubwa itakayofanyika Ukumbi wa Mliamni City jijini Dar es Salaam.
    Akizungumza na waandishi wa habari katika hafla ya uzinduzi wa tuzo hiyo ambayo imefanyika Keby's Hoteli iliyopo Bamaga jijini Dar es Salaam mchana huu, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, George Kavishe amesema wameboresha zaidi tuzo hizo ili kuzinogesha.
    Mambo mazuri zaidi; Meneja wa Bia ya Kilimanjaro, Geroge Kavishe akizungumza wakati wa uzinduzi wa tuzo wa Kili mwaka huu kwenye hoteli ya Keby's, Dar es Salaam.

    “Kuna maboresho makubwa ambayo mwaka huu tumefanya tofauti na mara zote ambazo tumekuwa tukihusisha Watanzania dakika za mwisho katika kupiga kura tu, hivyo kuwakosesha nafasi ya kupendekeza nani aingie kwenye 'category' (kipengele) gani. Mwaka huu tumebadilisha kutokana na matakwa ya soko, hivyo Watanzania ndiyo watapendekeza nani aingizwe kwenye category gani," amesema Kavishe.
    "Kupitia Magazeti, website ya Kilimanjaro na vipeperushi kuanzia kesho Februari 18 2014 kutaonyeshwa category zote za mwaka huu za kupigiwa kura na wananchi. Watanzania watatuma kura zao kupitia simu ya mkononi kupitia 15440, unapendekeza msanii, kikundi au producer gani aingie kwenye kipengele.
    “Kwa hiyo, mwaka huu Watanzania watapiga kura mara mbili; ya kwanza ni nani aingie kwenye category na ya pili tutarudi tena kupiga kura nani awe mshindi wa kwanza, yaani mwaka huu ile timu ya watu 100 ya waandishi, watangazaji na wadau wa muziki kuchagua nani na nani aingie kwenye category haitofanyika hivyo, bali itakutana kuhakikisha tu kama wimbo uliopendekezwa na wananchi ni wa mwaka husika, uko sehemu husika na pia kama umekidhi vigezo vya kuingia KTMA," amesema zaidi Kavishe.
    Wadau katika uzinduzi wa tuzo za Kili leo

    MABORESHO
    Kwa mujibu wa Baraza la sanaa la Taifa (BASATA) ambalo ndiyo mwandaaji wa tuzo hizo tangu zianzishwe 1999, mabadiliko yaliyofanywa kwenye tuzo za mwaka huu ni kutokana na maoni na mapendekezo ya wadau wa tasnia ya muziki kutoa sababu mbalimbali.
    Mratibu wa tuzo hizo kutoka baraza hilo, Kurwijira Ng'oko Maregesi, ambaye alikuwa amefuatana na Kavishe katika hafua ya leo mchana, amesema mwaka huu KTMA itakuwa na vipengele 36 ambapo category 34 ni za kuchaguliwa na mbili zilizobaki ni zile maalum za kuteuliwa.
    Maregesi amesema mwaka 2013 kulikuwa na vipengele 37, viwili vikiwa vya vya kuteuliwa lakini mwaka huu wameamua kuondoa kimoja kutokana na maoni mbalimbali ya wadau wa muziki. Kipengele kilichoondolewa ni Mtayarishaji Chipukizi wa Mwaka.
    Category zilizobadilishwa majina mwaka huu 2014 ni Mtumbuizaji bora wa Kike wa Muziki badala ya Msanii Bora wa Kike ilivyokuwa mwaka jana, Mtumbuizaji Bora wa Kiume wa Muziki badala ya Msanii Bora wa Kiume mwaka jana, Mwimbaji Bora wa Kiume Taarab ambayo mwaka jana ilikuwa Msanii Bora wa Kiume Taarab.
    Mwimbaji Bora wa Kiume Bongofleva badala ya mwaka jana Msanii Bora wa Kiume Bongofleva, Mwimbaji Bora Kiume Band ambayo mwaka jana ilikuwa Msanii Bora wa Kiume Band, Mwimbaji Bora wa Kike Bongofleva badala ya mwaka jana Msanii Bora wa Kike Bongofleva.
    Mwimbaji Bora wa Kike Taarab badala ya mwaka jana Msanii Bora wa Kike Taarab, Mwimbaji Bora wa Kike Band badala ya Msanii Bora wa Kike Band.
    "Ukiangalia maana halisi ya neno 'msanii' linasadifu au linaleta maana za kuingia zaidi ya kitu kimoja, kunaweza kuwapo msanii wa uchongaji, msanii wa uhoraji na wengineo, ndiyo maana tumeamua kutumia majina ya kimuziki kwa sababu huku tuko kwenye muziki," amesema Maregesi ambaye muda wote amesikika akizungumza Kiswahili Sanifu.
    Aidha, Maregesi amesema mwaka huu tutakuwa na Video Bora ya Muziki ya Mwaka badala ya Video Bora ya Wimbo kwa kuwa neno muziki lina uwanja mpana kuliko wimbo. Pia amesema kutakuwa na Wimbo Bora wa Afropop badala ya Wimbo Bora wa Bongopop, kutakuwa na Wimbo Bora Wenye Vionjo vya Asili ya Kitanzania badala ya Wimbo Bora Wenye Vionjo vya Asili ilivyokuwa mwaka jana.
    "Kutakuwa na kipengele cha Msanii Bora Chipukizi Anaeibukia badala ya Msanii Bora Anaechipukia kwa sababu wapo wasanii wengi sana chipukizi huko mtaani na miziki yao haijasikika," amesema.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TUZO ZA KILI 2014 ZAZINDULIWA LEO DAR, WAKALI KUJIBEBEA VYAO MEI 3 MLIMANI CITY Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top