• HABARI MPYA

    Sunday, December 30, 2012

    SIMBA SC WAONDOKA KESHO DAR

    Baadhi ya wachezaji wa Simba SC

    Na Mahmoud Zubeiry
    KIKOSI cha Simba SC kinaondoka kesho Dar es Salaam kwenda Zanzibar kwa ajili ya michuano ya Kombe la Mapinduzi, michuano inyaonza Jumanne.
    Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ aliiambia BIN ZUBEIRY jana kwamba timu hiyo itakuwa huko hadi baada ya mashindano, Januari 12 ndipo itaenda Oman kwa ziara ya wiki mbili.
    Simba SC jana ilicheza mechi ya kujipima nguvu na kufungwa mabao 3-0 na Tusker ya Kenya kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Katika mchezo huo, uliochezeshwa vema na refa Hashim Abdallah, hadi mapumziko, tayari Tusker walikuwa mbele kwa mabao 2-0, yaliyotiwa kimiani na Jesse Were dakika ya 37 na 45.
    Mabao yote yalitokana na udhaifu wa safu ya ulinzi ya Simba, ambayo hii leo iliongozwa na beki kutoka Mali, Komabil Keita kiasi cha kufikia mfungaji anafunga akiwa amebaki anatazamana na kipa.
    Simba ilikuwa ikishambulia kutokea pembeni, lakini mipira mingi mirefu iliyokuwa inamiminwa langoni mwa Tusker ilikuwa inaokolewa na mabeki warefu wa klabu hiyo bingwa ya Kenya, wakiongozwa na beki wa zamani wa Yanga, Joseph Shikokoti.
    Kipindi cha pili, Tusker walirudi kwa nguvu tena na kufanikiwa kupata bao la tatu dakika ya 54, mfungaji Frederick Onyango.
    Simba pamoja na kufanya mabadiliko, ikiwatoa Haruna Shamte, Haruna Athumani, Paul Ngalema, Mussa Mudde, Abdallah Seseme, Abdallah Juma, Ramadhani Chombo na Kiggi Makassy na kuwaingiza Miraj Adam, Hassan Isihaka, Emily Ngeta, Jonas Mkude, Salim Kinje, Haruna Moshi, Ramadhani Singano, Nassor Masoud ‘Chollo’ na Edward Christopher, haikuweza kupata hata bao la kufutia machozi.
    Nassor Masoud aliingia kuchukua nafasi ya Shamte, lakini naye akaumia na kutoka nafasi yake ikichukuliwa na kinda wa Simba, B, Masele Kaheza. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: SIMBA SC WAONDOKA KESHO DAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top