• HABARI MPYA

    Monday, December 31, 2012

    MCHEZAJI BORA CHALLENGE ATUA AZAM LEO

    Umony

    Na Prince Akbar
    MCHEZAJI bora wa Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge, Brian Umony anatarajiwa kuwasili leo mjini Dar es Salaam kujiunga na klabu yake mpya, Azam FC.
    Umony anawasili siku mbili tu, baada ya wachezaji wengine wapya wa Azam, kutoka Kenya, beki Joackins Atudo na kiungo Humphrey Mieno kuwasili Dar es Salaam kujiunga na klabu yao hiyo mpya.
    Nyota hao wote watatu, watakuwemo kwenye kikosi kitakachokwenda visiwani Zanzibar kesho kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi.
    Brian amerejea nyumbani Uganda mwaka huu na kujiunga na KCC baada ya kumaliza mkataba wake katika klabu ya Becamex Binh Duong F.C. ya Vietnam.
    Mwaka 2009, ilikuwa aje kuichezea Simba SC ya Dar es Salaam, lakini Wekundu hao wa Msimbazi wakazidiwa kete na SuperSport United ya Afrika Kusini.
    Umony aliichezea Supersport United hadi 2010 alipohamia University of Pretoria ya Afrika Kusini pia hadi mwaka 2011 alipohamia Portland Timbers ya Marekani kwa mkopo na mwaka huu akatua Becamex Binh Duong F.C. kabla ya kurejea Uganda na sasa anakuja kuanza maisha mapya Azam FC 2012.
    Kwa upande wa Atudo na Mieno, wao walianza kuichezea Azam katikati ya mwezi huu na walikuwepo kwenye kikosi cha timu hiyo kilichotwaa Kombe la Hisani la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), linaloandaliwa na FECOFA, Shirikisho la Soka la DRC wiki iliyopita, baada ya kuwachapa wenyeji, Dragons FC kwa penalti 4-2 kufuatia sare ya 2-2 ndani ya dakika 90.
    Azam iliingia fainali, baada ya kufanikiwa kuitoa kwa mikwaju ya penalti 5-4 Shark FC ya DRC Ijumaa, kufuatia sare ya 2-2 ndani ya dakika 90 kwenye Uwanja wa Martyrs.
    Kikosi kizima cha Azam kilichoshiriki mashindano hayo ni Kipre Tchetche, Seif Abdallah, Kipre Balou, Zahor Pazi, Jackson Wandwi, Malika Ndeule, Uhuru Suleiman, Omar Mtaki, Jabir Aziz, Ibrahim Mwaipopo, Gaudence Mwaikimba, Abdi Kassim, Luckson Kakolaki, Samih Hajji Nuhu, Mwadini Ally, Himid Mao, David Mwantika, Waziri Salum, Humphrey Mieno na Joackins Atudo.
    Katika mashindano hayo, Gaudence Mwaikimba aliibuka mfungaji bora kwa mabao yake matatu, ukiachilia mbali mawili ya penalti. Mchezaji mwingine wa kigeni wa Azam, Brian Umony wa Uganda, atajiunga na timu hiyo baada ya sikukuu pia.
    Azam wamepangwa Kundi B, katika Kombe la Mapinduzi pamoja na Mtibwa Sugar ya Morogoro, Coastal Union  ya Tanga na Miembeni ya Unguja.
    Kundi A lina timu za Simba SC, Tusker FC ya Kenya, Bandari ya Unguja na Jamhuri ya Pemba.
    Michuano ya Kombe la Mapinduzi, ambayo ni maalum kwa ajili ya kuherehekea Mapinduzi matukufu ya Zanzaibar, inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Januari 2, hadi kilele cha miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar, Januari 12, mwakani, huku ikishirikisha timu kutoka ndani na nje ya Tanzania.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: MCHEZAJI BORA CHALLENGE ATUA AZAM LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top