• HABARI MPYA

    Saturday, December 29, 2012

    MAJEMBE MAWILI AZAM NJE KOMBE LA MAPINDUZI

    Waziri Salum

    Na Prince Akbar
    VIUNGO wa Zanzibar, Waziri Salum na Abdulhalim Humud hawatacheza michuano ya Kombe la Mapinduzi, inayoanza wiki ijayo visiwani Zanzibar kutokana na kuwa bado majeruhi.
    Meneja Msaidizi wa Azam, Jemadari Said Kazumari aliiambia BIN ZUBEIRY jana kwamba, wawili hao hadi jana walikuwa hawajaripoti mazoezini, hivyo uwezekano wao wa kucheza michuano hiyo ni mdogo.
    Azam ambao ndio mabingwa watetezi wa taji hilo na mabingwa wa Kombe la Hisani la DRC, walianza mazoezi jana kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, baada ya mapumziko mafupi ya sikukuu ya Krisimasi.
    Katika maozezi hayo, wachezaji wengine watatu walikosekana, beki Joackins Atudo, kiungo Humphrey Mieno wote wa Wakenya na mshambuliaji Brian Umony wa Uganda kwa sababu bado wana udhuru hadi baada ya sikukuu ya Krisimasi.
    Azam ilitua Dar es Salaam Jumatatu usiku wiki hii, ikitokea Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ilikotwaa Kombe la Hisani, linaloandaliwa na FECOFA, Shirikisho la Soka la DRC.
    Azam walitwaa taji hilo Jumamosi iliyopita, baada ya kuwachapa wenyeji, Dragons FC kwa penalti 4-2 kufuatia sare ya 2-2 ndani ya dakika 90.
    Azam iliingia fainali, baada ya kufanikiwa kuitoa kwa mikwaju ya penalti 5-4 Shark FC ya DRC Ijumaa, kufuatia sare ya 2-2 ndani ya dakika 90 kwenye Uwanja wa Martyrs.
    Kikosi cha Azam kilichoshiriki mashindano hayo ni Kipre Tchetche, Seif Abdallah, Kipre Balou, Zahor Pazi, Jackson Wandwi, Malika Ndeule, Uhuru Suleiman, Omar Mtaki, Jabir Aziz, Ibrahim Mwaipopo, Gaudence Mwaikimba, Abdi Kassim, Luckson Kakolaki, Samih Hajji Nuhu, Mwadini Ally, Himid Mao, David Mwantika, Waziri Salum, Humphrey Mieno na Joackins Atudo.
    Katika mashindano hayo, Gaudence Mwaikimba aliibuka mfungaji bora kwa mabao yake matatu, ukiachilia mbali mawili ya penalti. Mchezaji mwingine wa kigeni wa Azam, Brian Umony wa Uganda, atajiunga na timu hiyo baada ya sikukuu pia.
    Azam wamepangwa Kundi B, katika Kombe la Mapinduzi pamoja na Mtibwa Sugar ya Morogoro, Coastal Union  ya Tanga na Miembeni ya Unguja.
    Kundi A lina timu za Simba SC, Tusker FC ya Kenya, Bandari ya Unguja na Jamhuri ya Pemba.
    Michuano ya Kombe la Mapinduzi, ambayo ni maalum kwa ajili ya kuherehekea Mapinduzi matukufu ya Zanzaibar, inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Januari 2, hadi kilele cha miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar, Januari 12, mwakani, huku ikishirikisha timu kutoka ndani na nje ya Tanzania.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: MAJEMBE MAWILI AZAM NJE KOMBE LA MAPINDUZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top