• HABARI MPYA

    Friday, December 28, 2012

    MFARANSA WA SIMBA SC ATAKUWAPO MECHI NA TUSKER JUMAMOSI TAIFA

    Liewig

    Na Prince Akbar
    KOCHA mpya wa mabingwa wa soka Tanzania Bara, Simba SC, Mfaransa Patrick Liewig atakuwapo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Jumamosi siku timu hiyo ikimenyana na mabingwa wa Kenya, Tusker FC.
    Ofisa Habari wa Simba SC, Ezekiel Kamwaga amesema kwamba, awali kocha huyo alitarajiwa kuawasili nchini jana, lakini imeshindikana baada ya kukosa nafasi kwenye ndege.
    Alisema kocha huyo ambaye anakuja kurithi mikoba ya Mserbia Profesa Milovan Cirkovick, atakishuhudia kikosi cha Simba kikicheza mechi hiyo kabla ya kuendelea na taratibu nyingine ikiwemo kusaini mkataba wa kazi na baadaye kuanza kutumikia kibarua chake kipya.
    Tusker FC ilianza vema ziara yake nchini, baada ya kuichapa Yanga 1-0 katika mchezo ulipigwa kwenye Uwanja wa Taifa juzi.
    Simba SC wamepangwa kundi moja, A na Tusker FC ya Kenya, Bandari ya Unguja na Jamhuri ya Pemba katika michuano ya Kombe la Mapinduzi, inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi hivi karibuni visiwani Zanzibar.
    Aidha, katika Kundi B, washindi wa pili wa Ligi Kuu ya Bara, Azam FC ya Dar e Salaam pia, imepangwa na Mtibwa Sugar ya Morogoro, Coastal Union  ya Tanga na Miembeni ya Unguja.
    Michuano ya Kombe la Mapinduzi, ambayo ni maalum kwa ajili ya kuherehekea Mapinduzi matukufu ya Zanzaibar, inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Januari 2, hadi kilele cha miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar, Januari 12, mwakani, huku ikishirikisha timu kutoka ndani na nje ya Tanzania.
    Kwa mujibu wa ratiba ya michuano hiyo iliyotolewa na Kamati Maalum ya Kusimamaia michuano hiyo, inaonesha kuwa katika mchezo wa kwanza utakaochezwa siku ya ufunguzi itakuwa ni kati ya Bandari kutoka Unguja ambayo itacheza na Jamhuri kutoka kisiwani Pemba ambao ni wawakilishi wa Zanzibar katika Kombe la Shirikisho Barani Afrika, pamabanolitakalochezwa katika uwanja wa Mao Tse Tung mjini Unguja, huku usiku wa siku hiyo hiyo katika Uwanja wa Amaan kisiwani Unguja pambano la ufunguzi rasmi katika mashindano hayo likiwakutanisha mabingwa wa soka nchini Tanzania, Simba SC ambao watapambana na mabingwa wa soka nchini Kenya, Tusker.
    Kwa mujibu wa ratiba hiyo jumla ya timu nane zitashiriki katika mashindano hayo ambayo yamejipatia umaarufu mkubwa visiwani hapa, timu hizo zimegawanya katika makundi mawili ambayo ni kama ifuatavyo:
    Awali michuano hiyo ilitarajiwa kuanza kisiwani Pemba tarehe 1 Januari, lakini kutokana na kujitoa katika mashindano kwa klabu ya Al-Ahly ya Misri kutokana na klie kilichoelezwa sababu za kiusalama, mechi zote sasa zitachezwa kisiwani Unguja na ufunguzi ukipangwa kuanza tarehe 2 badala ya tarehe 1 januari.
    Bingwa wa michuano hiyo ataondoka na zawadi ya kombe na fedha taslim Tsh.Milioni kumi (10,000,000), mshindi wa pili Milioni tano (5,000,000), pamoja na zawadi nyengine ambazo zimegawanywa katika makundi tofauti ikiwemo zawadi ya mfungaji bora, mchezaji bora, mwamuzi bora, kipa bora, mwandishi wa habari bora, timu bora na zawadi nyeanginezo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: MFARANSA WA SIMBA SC ATAKUWAPO MECHI NA TUSKER JUMAMOSI TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top