• HABARI MPYA

    Friday, December 21, 2012

    AZAM YATINGA FAINALI DRC

    Kipa Mwadini Ally kulia akimpongeza Nahodha wake, Jabir Aziz baada ya kufunga penalti ya mwisho

    Na Mahmoud Zubeiry, Kinshasa
    AZAM FC imefanikiwa kutinga Fainali ya Kombe la Hisani, baada ya kuifunga kwa mikwaju ya penalti 5-4 Shark FC ya hapa, kufuatia sare ya 2-2 ndani ya dakika 90 kwenye Uwanja wa Martyrs jioni hii.
    Nahodha Jabir Aziz Stima ndiye aliyekwenda kupiga penalti ya mwisho, Shark wakitoka kupoteza, kufuatia mpira kugonga mwamba. Aiziz aliwainua vitini wachezaji wenzake na makocha wake pamoja na viongozi wa wachache wa timu hiyo waliopo hapa kwa kupiga penalti maridadi iliyotinga nyavuni.
    Azam sasa, itamenyana na mshindi wa mechi inayoendelea hivi sasa kati ya Dragons na FC MK Jumapili katika fainali.
    Azam iliuanza mchezo huo vizuri na ikicheza kwa maelewano makubwa sambamba na kushambulia kwa kasi kutokea pembeni, kulia Kipre Herman Tchetche na kushoto Seif Abdallah.
    Hata hivyo, shambulizi la kushitukiza la Shark liliwapa bao la kuongoza dakika ya 16, lililofungwa na Ngulubi Kilua, baada ya mabeki wa Azam kudhani ameotea.
    Iliwachukua dakika 10 tu Azam kusawazisha bao hilo, mfungaji akiwa Gaudence Exavery Mwaikimba aliyeunganisha kwa kichwa krosi maridadi ya nyota wa mchezo wa leo, Kipere Herman Tcheche kutoka wingi ya kulia.
    Baada ya bao hilo, Azam iliendelea kuwashambulia Shark na dakika ya 37, Kipre Tchetche aliifungia timu hiyo bao la pili, kufuatia kazi nzuri ya Mwaikimba. Mwaikimba alipokea mpira mrefu, akatuliza na kumtangulizia kwa mbele mfungaji, ambaye hakufanya makosa, alimchambua kipa wa timu inayomilikiwa na mdogo wa rais wa DRC, Joseph Kabila.       
    Hadi mapumziko, Azam ilikuwa inaongoza kwa mabao 2-1 na kipindi cha pili Shark waliingia kwa kasi na kufanikiwa kusawazisha kwa penalti dakika ya 47, iliyotiwa nyavuni na Bukasa Kalambai, ambaye yeye mwenyewe alijiangusha kwenye eneo la hatari baada ya kuzongwa na beki David Mwantika.
    Baada ya dakika 90 kutimu timu hizo zikiwa zimefungana 2-2, sheria ya matuta ilichukua mkondo wake na wachezaji wote watano wa Azam waliopewa dhamana hiyo leo na kocha Muingereza Stewart Hall, walitimiza wajibu wao vizuri.
    Kipre Tchetche alifunga ya kwanza, Mwaikimba ya pili, Jaockins Atudo ya tatu, Himid Mao ya nne na Stima akapiga ya ushindi.
    Stewart alisema amefurahishwa na matokeo ya mchezo wa leo na sasa ana matumaini ya timu yake kurejea na Kombe hilo Dar es Salaam.
    Katika mchezo wa leo, kikosi cha Azam kilikuwa; Mwadini Ally, Himid Mao, Samih Hajji Nuhu, Joackins Atudo, David Mwantika, Jabir Aziz, Kipre Balou, Seif Abdallah/Uhuru Suleiman dk 77, Kipre Tchetche, Humphrey Mieno na Gaudence Mwaikimba.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: AZAM YATINGA FAINALI DRC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top