![]() |
| Minziro kulia akiwa na Samatta |
Na Mahmoud Zubeiry
FREDDY Felix Isaya Kataraiya ‘Minziro’ au Majeshi kwa jina lingine
la utani, kesho ataiongoza Yanga kwa mara ya pili mfululizo kama kocha Mkuu
kwenye mechi dhidi ya watani wa jadi, Simba SC, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Minziro amekuwa kocha Yanga kwa muda mrefu na kwa vipindi
tofauti, tangu mwaka 1997, lakini kwa kipindi chote hicho amekuwa Kocha
Msaidizi, ila dharula zilizojitokeza siku za karibuni zimekuwa zikimuangushia
kwenye kuaminiwa kuongoza timu katika mechi nzito.
Kama ilivyokuwa katika mechi iliyopita, Mei 6, mwaka huu, Minziro
aliachiwa timu wastani wa wiki mbili kabla ya mechi na watani na safari hii
inakuwa hivyo, ameachiwa timu ndani ya wastani wa muda huo.
Msimu uliopita, Minziro aliachiwa timu baada ya aliyekuwa
kocha wa timu hiyo, Mserbia Kostadin Bozidar Papic kutimuliwa, na safari hii
anaachiwa timu baada ya Mbelgiji, Tom Saintfiet pia kutimuliwa.
Ingawa Yanga imekwishaleta kocha mpya, Ernie Brandts kutoka
Uholanzi lakini rasmi bado hajaanza kazi kutokana na kutokamilishiwa kwa baadhi
ya taratibu za kikanuni- hivyo sana atakuwa na wasaa wa kutoa ushauri tu nje ya
Uwanja.
Jahazi kesho litaongozwa na Minziro, ambaye atakuwa akisaidiwa
na kocha wa makipa, Mfaume Athumani Samatta, wale wale waliopigwa 5-0 na Simba
SC. Mechi za Simba na Yanga zina ugumu wake kwa sababu zina mambo mengi sana.
Ingekuwa kazi rahisi kwa Minziro kukutana na Simba akiwa
kocha wa timu yoyote, lakini si Yanga na dhahiri usiku wa kuamkia kesho kwake
utakuwa mzito sana, akiitafakari mechi hiyo, na hasa akikumbuka zile 5-0 za Mei
6.
Mechi ya kesho itakuwa na sura mbili kwa Minziro, kumjenga au
kumbomoa mbele ya wana Yanga. Timu ikifanya vizuri itamjenga, lakini ikirudia
madudu ya Mei 6- hakika atakuwa kwenye wakati mgumu mno.
Dhahiri Yanga watamtazama mara mbili Minziro, kama kweli
wanaye kocha sahihi Msaidizi, ambaye anaweza kukaimu majukumu ya bosi wake
wakati wowote ikitokea dharula, au wana mtu tu kwenye benchi?
Kama itakumbukwa, staili kama hizi za kocha mkuu kupata
dharula ndizo zilimuinua Jamhuri Mussa Kihwelo ‘Julio’ pale Simba- kwani
aliachiwa timu na akawafunga Yanga Morogoro hata sasa naye amekuwa ‘Super Coach’.
Vivyo hivyo kwa Minziro, kesho itakuwa siku ya mtihani mzito
kwake, ambao vema kwake afaulu, lakini akifeli sijui awe na bahati gani tu hata
aendelee kuwa kocha wa Yanga.



.png)
0 comments:
Post a Comment