• HABARI MPYA

    Friday, October 26, 2012

    AZAM FC WAKO KAMILI, WAPANIA KUIPIGA SHOTI SIMBA KESHO

    Azam FC

    Na Mahmoud Zubeiry
    AZAM FC wamepania kuifunga Simba SC kesho katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ili kupanda kileleni mwa ligi hiyo.
    Kocha Boris Bunjak kutoka Serbia amekuwa akiwaandaa vizuri vijana wake kwa mazoezi na kisaikolojia pia kuelekea mchezo huo, unaotarajiwa kuwa mkali na wa kusisimua.
    Azam ipo kambini kwake, Chamazi ikijifua vikali na wachezaji wameweka kambi hapo, kwa ajili ya Ligi Kuu.
    Kiboko ya nyavu za Simba na Yanga, John Raphael Bocco ‘Adebayor’ yuko fiti kupita maelezo na kiungo bora Afrika Mashariki na Kati kwa sasa, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ aliyekuwa majeruhi mwanzoni mwa msimu sasa amepona kabisa.
    Kiungo Abdulhalim Humud aliyekuwa anasumbuliwa na maumivu katika mechi tatu zilizopita kwa sasa yuko fiti kabisa na habari njema zaidi ni kwamba, kiungo mwingine  Mzanzibari Abdi Kassim ‘Babbi’ amerudi kwenye fomu na anafumua mashuti makali na ya mbali ya hatari.
    Viungo washambuliaji kutoka Ivory Coast, Kipre Herman Tcheche na Kipre Michael Balou wote wapo fiti sawa na makipa Deo Munishi ‘Dida’, Mwadini Ally, mabeki Ibrahim Shikanda, Erasto Nyoni, Said Mourad na Aggrey Morris.
    Kwa ujumla Azam iko tayari kwa mechi hiyo ya kesho ambayo wamepania kushinda ili kulipa kisasi cha kufungwa na Simba katika Kombe la BancABC Sup8R.
    Simba yenyewe inaendelea vizuri na kambi yake visiwiani Zanzibar kujiandaa na mchezo huo na inatarajiwa kurejea kesho mchana na moja kwa moja kuelekea uwanjani kukipiga.   
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: AZAM FC WAKO KAMILI, WAPANIA KUIPIGA SHOTI SIMBA KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top