• HABARI MPYA

    Monday, October 22, 2012

    AZAM SASA WASHINDWE WENYEWE, UTAWALA WA LIGI UPO KWENYE HIMAYA YAO BAADA YA SIMBA KUCHEMSHA

    Azam FC

    Na Mahmoud Zubeiry
    AZAM FC inaweza kupanda kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Jumatano iwapo itaifunga Ruvu Shooting katika mfululizo wa ligi hiyo, kwani itafikisha pointi 20 baada ya kucheza mechi nane na bado itakuwa inazidiwa mchezo mmoja na vinara wa sasa wa ligi hiyo, Simba SC.
    Haya yatakuwa mabadiliko ya kwanza kileleni mwa ligi hiyo tangu kuanza kwake, Septemba 15 mwaka huu, kwani ni Simba imekuwa ikiongoza muda wote. Matumaini ya Azam kupaa kileleni Jumatano, yanafuatia jana Simba SC kulazimishwa sare ya 0-0 na wenyeji Mgambo JKT kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
    Simba sasa ina pointi 19, baada ya kucheza mechi tisa na Azam ina pointi 17, baada ya kucheza mechi saba, wakati Yanga iliyocheza mechi nane, ina pointi 14 katika nafasi ya tatu.
    Simba ilianza vema Ligi Kuu, ikishinda mechi tano mfululizo, lakini tangu itoe sare ya 1-1 na Yanga Oktoba 3, mwaka huu, ilishinda mechi moja tu kati ya nne zilizofuata, Oktoba 7, mwaka 2012 ilipoifunga 4-1 JKT Oljoro Uwanja wa Taifa.
    Mechi tatu zilizofuata Simba imetoa sare zote, bila kufungana na Mgambo na Coastal Union mjini Tanga na 2-2 na Kagera Sugar, Uwanja wa Taifa. 
    Kocha Bunjak kushoto akijadiliana jambo na Meneja wa Azam, Patrick Kahamele wakati wakiifuatilia Ruvu Shooting ilipokuwa ikicheza na Yanga Jumamosi Uwanja wa Taifa
    Hadi sasa, Azam na Simba ndio timu pekee ambazo hazijafungwa katika Ligi Kuu na hii inaashiria kwamba bado hizo ndizo timu bora katika ligi hiyo, zikiendeleza upinzani wao wa tangu msimu uliopita.
    Msimu uliopita, Simba ilitwaa ubingwa na Azam ikawa ya pili, wakati Yanga iliambulia nafasi ya tatu na hadi sasa katika msimamo wa Ligi Kuu, mpangilio uko hivyo ingawa ni matarajio ya wengi keshokutwa mambo yatabadilika.
    Lakini pia mbele ya Ruvu Shooting iliyoonyesha upinzani mkubwa ikicheza na Simba na Yanga na kufungwa kwa tabu, tena kukiwa na dalili za wapinzani wao kubebwa kidogo na marefa katika mechi zote, hilo linaweza kuwa gumu.
    Kitu kimoja tu, Azam imekuwa na rekodi nzuri kwenye Uwanja wake, Chamazi na kwa sababu keshokutwa kipute kitapigwa hapo, timu hiyo ya Said Salim Bakhresa na familia yake inaweza kupaa kileleni.
    Azam ni bora, na ndiyo maana kila mashindano inayoshiriki tangu mwaka jana imekuwa ikifika mbali.  Ina Medali za Fedha za Ligi Kuu, Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame na Kombe la Urafiki na pia hawa ni mabingwa wa Kombe la Mapinduzi.   
    Wawakilishi hao wa Tanzania kwenye Kombe la Shirikisho mwakani, wanajivunia kikosi chao kizuri chenye wachezaji bora kama mfungaji bora wa Ligi Kuu, John Bocco ‘Adebayor’, Kipre Tchetche, Salum Abubakar ‘Sure Boy Jr.’ na wengineo.
    Lakini pia kocha mtaalamu, hodari na mchapakazi, Mserbia, Boris Bunjak ambaye Jumamosi alikuwapo Uwanja wa Taifa kuitathmini Ruvu Shooting ilipokuwa ikicheza na Yanga na kufungwa kwa mbinde 3-2.
    Hadi sasa Bunjak ameiongoza Azam FC katika mechi 14, kati ya hizo saba za Ligi Kuu, ambazo ameshinda tano na kutoa sare mbili, zote ugenini 2-2 na Toto African mjini Mwanza na 0-0 na Prisons mjini Mbeya.
    Timu moja tu ambayo imemfunga Bunjak hadi sasa, Simba SC katika mechi tatu, moja ya michuano ya BancABC Sup8R, 2-1, Ngao ya Jamii 3-2 na mchezo wa kirafiki 3-2 pia. Kwa ujumla kulingana na mwenendo wa Ligi Kuu hadi sasa, Azam ikiwa imecheza mechi saba, imeonyesha msimu huu ‘haitaki masihara’.

    REKODI YA BORIS BUNJAK AZAM
    Azam 2-1 Polisi                    (BancABC)
    Azam 2-1 Simba B              (BancABC)
    Azam 8-0 Trans Camp       (Kirafiki)
    Azam 1-0 Prisons                (Kirafiki)
    Azam 2-0 Coastal Union   (Kirafiki)
    Azam 2-3 Simba SC            (Ngao ya Jamii)
    Azam 1-0 Kagera Sugar     (Ligi Kuu)
    Azam 2-2 Toto African      (Ligi Kuu)
    Azam 3-0 JKT Ruvu             (Ligi Kuu)
    Azam 1-0 Mtibwa Sugar    (Ligi Kuu)
    Azam 1-0 African Lyon      (Ligi Kuu)
    Azam 2-3 Simba SC            (Kirafiki)
    Azam 1-0 Polisi                    (Ligi Kuu)
    Azam 0-0 Prisons                (Ligi Kuu)                              
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: AZAM SASA WASHINDWE WENYEWE, UTAWALA WA LIGI UPO KWENYE HIMAYA YAO BAADA YA SIMBA KUCHEMSHA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top