• HABARI MPYA

    Tuesday, October 23, 2012

    SIMBA WAENDA ZANZIBAR KUIANDALIA KIPIGO AZAM

    Wachezaji wa Simba

    Na Princess Asia
    SIMBA SC imefanya mazoezi kwenye ufukwe wa Coco leo asubuhi na wachezaji wote wameruhusiwa kurudi manyumbani kwao, kujiandaa kwa safari ya Zanzibar jioni kwenda kuweka kambi ya kujiandaa na mechi dhidi ya Azam FC Jumamosi wiki hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Kwa kawaida Simba SC huenda Zanzibar katikati ya Ligi Kuu kuweka kambi linapokaribia pambano dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Yanga SC lakini kwa kitendo cha kwenda kujichimbia huko kwa ajili ya Azam, maana yake wanaipa uzito huo mechi hiyo.
    Kikosi cha Simba kilirejea Dar es Salaam jana mchana kutoka Tanga ambako kilitoka sare ya bila kufungana na wenyeji Mgambo JKT Jumapili katika mfululizo wa ligi hiyo.
    Matokeo hayo, yanaifanya Simba ifikishe pointi 19, baada ya kucheza mechi tisa na kuendelea kuongoza Ligi Kuu, ingawa wameuweka rehani usukani wa ligi hiyo kwa Azam ambayo kesho inacheza na Ruvu Shooting Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.
    Awali ya hapo, Simba ilitoka 2-2 na Kagera Sugar Uwanja wa Taifa na 0-0 na Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani.
    Azam yenye pointi 17, ikishinda itafikisha pointi 20 na kupanda kileleni, tena ikiwa nyuma kwa mchezo mmoja, kwani hadi sasa imecheza mechi saba. Yanga iliyocheza mechi nane, ina pointi 14 katika nafasi ya tatu nayo itacheza na Polisi Morogoro keshokutwa.
    Baada ya sare ya Jumapili, Mwenyekiti wa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage amewataka wanachama na wapenzi wa klabu hiyo kuwa watulivu na wasikatishwe na tamaa na sare tatu mfululizo za timu hiyo katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kwani safari bado ni ndefu.
    Rage amesema kwamba, hadi sasa timu yao haijafungwa katika Ligi Kuu kuashiria kwamba bado ni timu bora na matokeo ya sare hizo tatu mfululizo pia ni kutokana na uimara wa timu yao.
    Rage ameonya wanachama wenye desturi ya kutoa maneno ya uchochezi timu inapoyumba kidogo, waache kufanya hivyo kwa sababu wanaweza kuvuruga amani iliyopo sasa klabuni.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: SIMBA WAENDA ZANZIBAR KUIANDALIA KIPIGO AZAM Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top