• HABARI MPYA

    Saturday, October 27, 2012

    SIMBA MATAWI YA JUU, YANGA YAENDELEZA WIMBI LA USHINDI

    Wachezaji wa Simba kwa raha zao


    Na Mahmoud Zubeiry
    SIMBA SC imezinduka kutoka kwenye wimbi la sare katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya kufanikiwa kuichapa Azam FC mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Ushindi huo, unaifanya Simba izidi kujitanua kileleni mwa ligi hiyo kwa kufikisha pointi 22, baada ya kucheza mechi 10, wakati Azam FC inapromoka hadi nafasi ya tatu kwa pointi zake 18, baada ya kucheza mechi tisa, ikiipisha Yanga nafasi ya pili, ambayo imetimiza pointi 20 baada ya kuifunga JKT Oljoro leo.
    Mabao ya Simba leo yalitiwa kimiani na Emanuel Arnold Okwi mawili na Felix Mumba Sunzu Jr. moja, wakati la Azam lilifungwa na John Raphael Bocco ‘Adebayor’.
    Hadi mapumziko, tayari Simba walikuwa mbele kwa mabao 2-1, Azam wakitangulia kufunga dakika ya nne, kupitia kwa Adebayor ambaye alimtoka beki Mkenya Paschal Ochieng na kumchambua Juma Kaseja.
    Dakika mbili baadaye, Sunzu aliisawazishia Simba, akiunganisha kwa kichwa krosi maridadi ya Mrisho Khalfan Ngassa kutoka wingi ya kulia.
    Okwi aliifungia Simba bao la pili dakika ya 40, baada ya kutokea kizaazaa langoni mwa Azam kufuatia mpira uliopigwa langoni mwa timu hiyo na Mwinyi Kazimoto.     
    Kipindi cha pili Simba walirudi na moto wao na iliwachukua dakika tano tu kuhitimisha karamu yao ya mabao, baada ya Okwi kuwainua tena vitini mashabiki wa Simba, akifumua shuti la umbali wa mita 19, baada ya kuwatoka mabeki wa Azam.
    Mrisho Ngassa ndiye alikuwa nyota wa mchezo wa leo, kutokana na kuisumbua mno Azam, iliyomuuza kwa mkopo Simba miezi miwili iliyopita.
    Simba SC; Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’, Amir Maftah, Paschal Ochieng, Shomary Kapombe, Jonas Mkude, Amri Kiemba/Ramadhan Chombo, Mwinyi Kazimoto, Felix Sunzu/Ramadhan Singano, Mrisho Ngassa/Christopher Edward na Emmanuel Okwi.
    Azam FC; Mwadini Ali, Ibrahim Shikanda, Samir Hajji Nuhu, Said Mourad na Aggrey Morris, Abdulhalim Humud, Jabir Aziz/Abdi Kassim, Himid Mao/Kipre Balou, John Bocco ‘Adebayor’/Khamis Mcha, Kipre Herman na Salum Abubakar.
    Katika mchezo uliotangulia, Azam B iliifunga Simba B 1-0, bao pekee la Kevin Friday dakika ya 56.
    Kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha, Yanga iliibuka na ushindi wa 1-0, bao pekee la beki Mbuyu Twite, hilo likiwa bao lake la tatu tangu ajiunge na timu hiyo kwenye ligi hiyo.
    Kwa ushindi huo, Yanga imetimiza pointi 20, baada ya kucheza mechi 10 na kupanda nafasi ya pili.
    Mechi nyingine za ligi hiyo leo ni kati ya African Lyon imetoka sare ya 1-1 Kagera Sugar Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam, Ruvu Shooting imeifunga 2-1 Polisi Morogoro Uwanja wa Mabatini, Mlandizi.
    Mechi kati ya Mgambo JKT na Prisons iliyokuwa ichezawe leo Uwanja wa Mkwakwani, Tanga imeahirshwa kutokana na wachezaji wa Prisons kupata ajali wakiwa njiani kuelekea Tanga.
    Ligi hiyo itaendelea kesho kwa michezo miwili kati ya JKT Ruvu na Coastal Union Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam na Toto Africans dhidi ya Mtibwa Sugar Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: SIMBA MATAWI YA JUU, YANGA YAENDELEZA WIMBI LA USHINDI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top