• HABARI MPYA

    Tuesday, October 23, 2012

    UKUTA WA AZAM WATIA FORA LIGI KUU, BORA 'DIFENSI' YA MGAMBO KULIKO SIMBA NA YANGA

    Azam FC; Wenye ukuta tishio zaidi Ligi Kuu

    Na Mahmoud Zubeiry
    WAKATI Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ipo katika mzunguko wake wa tisa, hadi sasa Azam FC ndio imeonyesha kuwa timu yenye ukuta mgumu zaidi na ikiwa kesho inamenyana na Ruvu Shooting katika mfululizo wa ligi hiyo, imefungwa mabao mawili tu katika mechi saba.
    Azam ilifungwa mabao hayo katika mechi yake ya pili, dhidi ya wenyeji Toto African kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza na tangu hapo imecheza dakika 450 bila kuruhusu nyavu zao kutikiswa na katika mechi zote hizo alidaka Mwadini Ally.
    Kwa kawaida safu ya ulinzi ya Azam huwa haibadiliki sana na katika mechi zote hizo ambazo hawajafungwa, Mwadini amekuwa akilindwa na Ibrahim Shikanda kulia, kushoto Erasto Nyoni na katikati Aggrey Morris na Said Mourad, juu yao kiungo mkabaji Ibrahim Mwaipopo.
    Unasemaje kuhusu ukuta huu, upo ukuta unaostahili kuitwa jina gumu katika Ligi Kuu hadi sasa zaidi ya huu? Hakuna hakika.
    Kasi ya ufungaji wa mabao ya Azam hadi sasa ni ya wastani wa kati, katika mechi saba walizocheza wamefunga mabao manane, bado ni wastani wa bao moja katika kila mechi na hii ni kwa sababu mfungaji bora wa timu hiyo, John Bocco ‘Adebayor’ bado hajafunguka.
    Kwa wenye kufuatilia rekodi ya Bocco katika Ligi Kuu, amekuwa tishio zaidi katika mzunguko wa pili, hivyo bado hatuwezi kusema chochote juu yake hadi sasa hadi wakati utakapofika.
    Timu inayoifuatia Azam kwa kuwa na ukuta mgumu ni JKT Mgambo Shooting, ambao wamepanda Ligi Kuu msimu huu. Timu hiyo ya Muheza, katika mechi zake nane ilizocheza hadi sasa, imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara nne tu, ingawa na yenyewe pia haina makali sana ya kufunga, kwani imefunga mabao sita tu.
    Ingawa haijafunga hata bao moja katika Ligi Kuu msimu huu, Polisi ya Morogoro iliyopanda pia Ligi Kuu msimu huu, ni timu ya tatu kwa ubora wa beki yake hadi ligi ilipofikia, hadi sasa katika mechi zake sita wamefungwa mabao matano tu. Hii ni timu ambayo inashika mkia katika Ligi Kuu na kesho inamenyana na Yanga.
    Prisons ya Mbeya ambayo nayo imepanda Ligi Kuu msimu huu, pia ina ukuta mgumu, kwani katika mechi zake nane ilizocheza hadi sasa, imefungwa mabao matano tu, ingawa nayo pia haina safu tishio sana ya ufungaji, kwani imefunga mabao matano pia.
    Tazama utaona timu zote zilizopanda Ligi Kuu msimu huu zimewekeza vizuri katika safu zake za ulinzi- Mgambo, Prisons na Moro, zote zimefungwa mabao machache kuliko hata vigogo Simba na Yanga waliotumia mamilioni mengi kusajili hadi mabeki wa kigeni.
    Mabingwa watetezi Simba SC, wakiwa wanaongoza kwa safu kali zaidi ya ushambuliaji, iliyovuna mabao 16 katika mechi tisa, ndiyo wanaofuatia kwa kuwa na ukuta mgumu, wakiwa wamefungwa mabao sita tu katika mechi hizo.
    Kagera Sugar ya Bukoba ndiyo inayofuatia kuwa na ukuta mgumu, ikiwa imefungwa mabao sita pia katika mechi zake saba na yenyewe imefunga mabao saba.
    Coastal Union ya Tanga katika mechi zake nane, pia imefungwa mabao manane, wakati yenyewe imefunga mabao 10, sawa na JKT Oljoro ambayo katika mechi nane pia, imefunga mabao nane, ingawa yenyewe imefunga mabao saba wakati Mtibwa Sugar katika mechi saba imefunga mabao manane na imefungwa manane pia.
    Yanga ndiyo wanafuatia sasa kwa ‘ukuta bora’, wakiwa wamefungwa mabao 10 katika mechi nane, ingawa hawa sasa wanaonekana pia kuwa na safu kali ya ushambuliaji, ambayo hadi sasa imefunga mabao 14.
    Hiyo ni safu ya ushambuliaji ya pili kwa ukali wa mabao, baada ya safu ya mabingwa watetezi Simba SC, iliyofunga mabao 16 hadi sasa katika mechi tisa.
    African Lyon inafuatia kuwa na safu kali ya ulinzi, katika mechi nane ikiwa imefungwa mabao 11 na hatari zaidi ni kwamba hata safu yake ya ushambuliaji haitishi sana, kwani imefunga mabao matano tu.
    Toto African ambayo ndio pekee inajua utamu wa nyavu za Azam hadi sasa, nayo imefungwa mabao 11 katika mechi nane, ikiwa nayo imefunga mabao matano tu.
    Timu mbili za mkoa mmoja, Pwani, Ruvu Shooting na JKT Ruvu ndizo ambazo zinaongoza kuwa na kuta zenye nyufa nyingi, kwani hadi sasa zimeruhusu mabao 13 kila timu.
    Ruvu Shooting pamoja na kufungwa mabao 13, angalau nayo imeonyesha uhai katika safu yake ya ushambuliaji kwa kufunga mabao 11, lakini JKT iliyofungwa ‘dazeni’ ya mabao na nyongeza ya bao moja, yenyewe imefunga mabao saba tu.
    Katika msimamo wa Ligi Kuu, mbio za ubingwa hadi sasa bado ni za farasi watatu tu, Simba, Yanga na Azam zinazofukuzana kileleni, wakati kule kwenye mlango wa kutokea, Mtibwa Sugar, JKT Ruvu, African Lyon, Toto African na Polisi Moro zimebanana kisawasawa. Yote tisa, ukuta wa Azam umetia fora hadi sasa katika Ligi Kuu na safu ya ushambuliaji ya Simba ndiyo inayotisha zaidi.

    MSIMAMO WA LIGI KUU BARA
                                  P    W  D   L    GF GA GD Pts
    Simba SC               9    5    4    0    16 6    10 19
    Azam FC                7    5    2    0    8    2    7    17
    Yanga SC               8    4    2    2    14 10 4    14
    Coastal                   8    3    3    2    10 8    2    13
    JKT Oljoro              8    2    5    2    7    8    -1  11
    JKT Mgambo          8    3    2    3    6    4    2    10
    Prisons                   8    2    4    2    5    5    0    10
    Kagera Sugar         7    2    3    2    7    6    1    9
    Ruvu Shooting        8    3    0    5    11 13 -2  9
    Mtibwa Sugar          7    2    2    3    8    8    0    8
    JKT Ruvu                8    2    2    4    7    13 -6  8
    African Lyon            8    2    1    5    5    11 -6  7
    Toto African             8    1    3    4    7    11 -4  6
    Polisi Moro               6    0    2    4    0    5    -5  2
    (P idadi ya mechi ambazo timu imecheza, W mechi ambazo imeshinda, D sare, L kufungwa, GF mabao iliyofunga, GA mabao iliyofungwa, GD mabao iliyonayo ukitoa mabao iliyofungwa, -maana yake imefungwa zaidi ya ilivyofunga na Pts ni idadi ya pointi)
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: UKUTA WA AZAM WATIA FORA LIGI KUU, BORA 'DIFENSI' YA MGAMBO KULIKO SIMBA NA YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top