• HABARI MPYA

    Thursday, October 25, 2012

    YANGA WAENDA ARUSHA ALFAJIRI YA LEO

    Wachezaji wa Yanga

    Na Mahmoud Zubeiry
    YANGA SC imeondoka leo alfajiri Dar es Salaam na kikosi cha wachezaji 20 kwenda Arusha kwa ajili ya mechi yao ya Jumamosi dhidi ya wenyeji JKT Oljoro kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha.
    Wachezaji waliokwenda Arusha leo ni makipa Yaw Berko, Ally Mustafa ‘Barhez’, mabeki, Oscar Joshua, Juma Abdul, David Luhende, Stefano Mwasyika, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ (Nahodha), Mbuyu Twite na Kelvin Yonda.
    Viungo ni Athumani Iddi ‘Chuji’, Frank Domayo, Rashid Gumbo, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Nurdin Bakari, Nizar Khalfan, Juma Seif ‘Kijiko’ na washambuliaji Jerry Tegete, Hamisi Kiiza na Didier Kavumbangu.
    Yanga inakimbilia Arusha mapema ili kuwahia kuzoea hali ya hewa ya huko, wasije kupata tabu katika mchezo wa Jumamosi.
    Mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu, wanakwenda Arusha wakitoka kuendeleza wimbi la ushindi jana katika Ligi Kuu, baada ya kuichapa Polisi Morogoro mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Ushindi huo, unaifanya Yanga itimize pointi 17, baada ya kucheza mechi tisa na kuendelea kusimama katika nafasi ya tatu, nyuma ya Azam FC yenye pointi 18, baada ya sare ya 1-1 na Ruvu Shooting Uwanja wa Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.  
    Hadi mapumziko jana, Yanga walikuwa mbele kwa mabao 2-0 yaliyotiwa kimiani na washambuliaji Simon Msuva na Didier Kavumbangu.
    Msuva alikuwa wa kwanza kuwainua vitini mashabiki wa Yanga dakika ya tano kabla ya dakika moja baadaye, Mrundi Kavumbangu naye kuwapa raha mashabiki wa timu hiyo.
    Yanga ingekwenda kupumzika ikiwa inaongoza kwa mabao 3-0 kama mkwaju wa penalti wa Haruna Niyonzima usingegonga mwamba na kurudi uwanjani kabla ya mabeki wa Polisi kuondosha kwenye hatari.
    Refa Alex Mahagi kutoka Mwanza alitoa penalti hiyo, baada ya Msuva kuangushwa na beki John Bosco kwenye eneo la hatari wakati anakwenda kufunga.    
    Kipindi cha pili Yanga walirudi kwa kasi tena na kuendelea kulishambulia lango la Polisi, ingawa walipoteza nafasi nyingi na kutumia moja tu, dakika ya 58, mfungaji Hamisi Kiiza aliyeingia kuchukua nafasi ya Jerry Tegete.
    Matokeo ya jana yanaziweka karibu mno, Simba inayoongoza kwa pointi zake 19 baada ya kucheza mechi tisa, Azam na Yanga pale juu, kiasi kwamba ushindani na uhondo wa ligi hiyo unaongezeka.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: YANGA WAENDA ARUSHA ALFAJIRI YA LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top