• HABARI MPYA

    Wednesday, July 08, 2015

    BOCCO: SITAKI KWENDA KUCHEZA NJE KWA SIFA, MASLAHI MUHIMU

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    NAHODHA wa Azam FC, John Raphael Bocco ‘Adebayor’ (pichani) amesema kwamba hajakataa ofa ya kwenda Free State Stars ya Afrika Kusini, bali kuna mambo mengi hakuridhika nayo katika mjadala wa Mkataba.
    “Wakala ambaye alikuwa anashughulikia suala langu hakunipa nafasi ya kuzungumza moja kwa moja na klabu. Lakini hiyo si kitu. Ofa waliyonipa sikuridhika nayo,”amesema.
    Bocco amesema kwamba kitu kikubwa kwa mchezaji ni maslahi na si kucheza wapi. “Asamoah Gyan aliondoka Uingereza akaenda Uarabuni kucheza kwa sababu ya maslahi. Hata mimi kama ninaona hapa Azam FC ninapata maslahi bora kwa nini niende sehemu ambayo siridhiki na maslahi,”amesema.
    Bocco amewataka Watanzania wamuelewe kwamba kwa muda mrefu amekuwa akihangaikia kupata nafasi ya kucheza nje na ndiyo maana alikwenda Afrika Kusini mara mbili, Israel na Algeria kote kutafuta timu.
    “Mimi nimekwenda Afrika Kusini mara mbili na mara zote nimefanya vizuri, lakini SuperSport wakashindwa kumalizana na Azam. Nilikwenda Israel pia na Algeria kote nilifanya vizuri, lakini klabu zikashindwa kumalizana vizuri na Azam,”amesema Bocco na kuongeza.
    “Hata sasa kama inatokea nafasi na maslahi yanakuwa mazuri ninakwenda, sitaki kwenda nje kwa sifa, eti nipo Afrika KUsini au wapi, halafu maslahi yenyewe hayaeleweki,”amesema.
    Azam FC ilikubali kumuuza mshambuliaji wake huyo kwa dola za Kimarekani 80,000 zaidi ya Sh. Milioni 160 za Tanzania kwa klabu ya Free State Stars.
    Lakini Bocco amekataa kwa sababu ambazo amezieleza na FS ambayo Mei mwaka huu ilimsajili Mtanzania, mwingine Mrisho Ngassa imemuita Mganda Frank Kalanda wa URA kwa majaribio achukue nafasi hiyo.
    Kwa sasa FS wapo kambini katika hoteli ya Lake View mjini Johannesburg kujiandaa na Ligi Kuu ya Afrika Kusini, inayotarajiwa kuanza Agosti 8, mwaka huu.
    Timu hiyo ya kocha Mmalawi, Kinnah Phiri inatarajiwa kuanza na Black Aces, wakati mechi ya pili watacheza na mabingwa watetezi, Kaizer Chiefs. Mechi ya kwanza, Kaizer wataanza kutetea taji lao dhidi ya Chippa United Agosti 8.
    Kwa mujibu wa ratiba ya msimu wa PSL wa 2015-16, Mamelodi Sundowns wataanza na Platinum Stars, Orlando Pirates na SuperSport United, wakati timu mbili zilizopanda msimu huu, Golden Arrows na Jomo Cosmos watakuwa nyumbani na University ya Pretoria na ugenini na Maritzburg United.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BOCCO: SITAKI KWENDA KUCHEZA NJE KWA SIFA, MASLAHI MUHIMU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top