• HABARI MPYA

    Sunday, June 07, 2015

    MFARANSA ALIYEIPELEKA NUSU FAINALI AFRIKA COTTON SPORT ATAJWA SIMBA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    KOCHA Mfaransa, Didier Gomez de Roza ametajwa kuwa ndiye anayekuja kufundisha Simba SC, lakini Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hans Poppe amesema; “Si huyo”, ila hajamtaja mwingine.
    Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) amesema kocha huyo hayupo kabisa katika mipango yao.
    Lakini mapema leo, chanzo cha habari kimesema kwamba Mfaransa huyo aliyewahi kufundisha Rayon Sport ya Rwanda ndiye anakuja Simba SC.  
    Mfaransa huyo ana rekodi nzuri na mwaka jana alikuwa Cotton Sport ya Gorua, Cameroon ambayo aliifikisha Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
    Didier Gomez de Roza ametajwa kuwa anakuja Simba SC
    Lakini Hans Poppe kushoto amemkana mwalimu huyo

    Hans Poppe amesema; “Mchakato wetu wa kocha unaendelea vizuri na tutakapokamilisha kila kitu tutamtangaza, ila si huyo unayesema wewe na si Mfaransa kabisa,”.
    Hans Poppe ameihakikishia BIN ZUBEIRY kwamba Mserbia, Goran Kopunovic hatarejea Msimbazi.
    Kopunovic aliyeiongoza Simba SC kwa nusu ya pili ya msimu uliopita, baada ya kumaliza Mkataba wake wa miezi sita alishindwana dau la Mkataba mpya na Wekundu hao wa Msimbazi.
    Baadaye ikaripotiwa, Goran alijishusha na kuwa tayari kurejea Msimbazi kufanya kazi, lakini wakati huo tayari uongozi wa Simba SC ulikuwa umekwishaingia kwenye mchakato wa kocha mpya.
    Kitendawili ni bado nani atakuwa kocha mpya wa Simba SC kuelekea msimu ujao- ikiwa Hans Poppe amemkana Mfaransa Didier Gomez de Roza? 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MFARANSA ALIYEIPELEKA NUSU FAINALI AFRIKA COTTON SPORT ATAJWA SIMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top