• HABARI MPYA

    Sunday, June 28, 2015

    TAIFA STARS YA BAADAYE YAWAFUMUA MBEYA KOMBAINI 3-0 SOKOINE

    Na Mahmoud Zubeiry, MBEYA
    TIMU ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 15, jioni ya leo imeibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Kombaini y vijana chini ya umri wa 17 ya Mbeya Uwanja wa Sokoine mjini hapa.
    Katika mchezo huo uliohudhuriwa na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Emil Malinzi dakika 45 za kwanza zilimalizika U15 wakiwa mbele kwa bao 1-0.
    Bao hilo lilifungwa na mshambuliaji Timoth Maziku dakika ya 17 kwa guu la kulia akimalizia krosi ya Nahodha Issa Abdi.
    Baada ya bao hilo, Mbeya Kombaini walitulia na kuanza kusukuma mashambulizi langoni mwa timu ya taifa, hali ambayo ilifanya timu hizo zishambuliane kwa zamu huku pia vijana wakionyesha uwezo wa kuridhisha.
    Nahodha wa U15 ya taifa, Issa Abdi (katikati) akishangilia na wenzake baada ya kufunga bao la pili
    Issa Abdi akiruka kwanja la beki wa Mbeya
    Kocha wa U15, Bakari Shime akiwapa maelekezo wachezaji wake wakati wa mapumziko mafupi ya mchezo huo kupisha kipa wa Mbeya apatiwe huduma ya kwanza
    Rais wa TFF, Jamal Malinzi (katikati) akisalimiana na wachezaji wa Mbeya Kombaini kabla ya mchezo huo

    Dakika ya 72, Albinius Haule almanusra aisawazishie bao Mbeya kama si shuti lake zuri la kitaalamu alilopiga kutoka umbali wa mita 25 kugonga mwamba wa juu na kutoka nje.
    Nahodha Issa Abdi aliifungia timu ya taifa bao la pili dakika ya 82 kwa shuti la mpira wa adhabu baada ya Timoth Maziku kuangushwa nje kidogo ya boksi na Richard Paul.
    Emmanuel Ntindi wa Mbeya alijifunga dakika ya 87 katika harakati za kuokoa krosi ya Asad Ally dhidi ya Maziku.
    Mchezo ulikuwa mzuri, vijana walionyesha ufundi wa hali ya juu- na Mbeya pamoja na kufungwa, ilicheza vizuri na kilichowakwamisha kupata japo bao moja ni uhodari wa kipa Kelvin Deogratius wa U15 ya taifa.
    Timu hizo zinatarajiwa kurudiana kesho jioni kwenye Uwanja huo huo na mapema Jumanne U15 itarejea Dar es Salaam na vijana kuvunja kambi hadi watakapokusanywa tena mwishoni mwa mwezi ujao kwa safari ya Zanzibar kwa michezo mingine ya kujipima.
    Vijana hao walio chini ya kocha Bakari Shime wanaandaliwa kwa ajili ya kucheza mechi za kufuzu Fainali za Vijana Afrika chini ya umri wa miaka 17 mwaka 2017 na kila wiki ya mwisho wa mwezi watakuwa wakikutana kwa mazoezi na michezo ya kujipima nguvu.
    Kikosi cha Mbeya Kombaini kilikuwa; Edward Mwakyusa, Josephat Frank, Seif Gabriel, Emmanuel Ntindi, Richard Paul/Hassam Abdallah dk87, Goodluck Ezeria, Amiri Nyeo, Castro Issa, Albinius Haule, Biya Stephen na Daniel Samson/Castro Moses dk73.
    Tanzania U15; Kelvin Deogratius, Kibwana Ally, Faraji John, Maulid Salum, Ally Hussein, Athumani Maulid/Rashid Kilomtola dk75, Robert Philipo/Morris Michael ‘Chuji’ dk86, Asad Ally, Timoth Joseph, Issa Abdi na Juma Zubeiry/Juma Juma dk61.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TAIFA STARS YA BAADAYE YAWAFUMUA MBEYA KOMBAINI 3-0 SOKOINE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top