• HABARI MPYA

    Sunday, June 28, 2015

    ULIMWENGU: SIKUFIKIRIA ERASTO NYONI ANGEACHWA TAIFA STARS

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MSHAMBULIAJI wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Thomas Emmanuel Ulimwengu (pichani) amesema hakufikiria kabisa kama beki Erasto Edward Nyoni angeachwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY kwa simu jana kutoka Lubumbashi, Ulimwengu alisema kwamba amesikia mabadiliko yaliyofanyika katika timu ya taifa, kocha Mholanzi Mart Nooij akiondolewa na nafasi yake kuchukuliwa na mzalendo Charles Boniface Mkwasa.
    Hakuwa na maoni yoyote juu ya mabadiliko hayo, ila kuhusu kikosi kilichoundwa na Mkwasa baada ya kupewa madaraka, amesema; “Sikufikiria kabisa kama Erasto angeachwa, ila ndiyo soka,”amesema.
    Ulimwengu amesema kwa upande wake yuko tayari kufanya kazi na mwalimu yeyote popote na kwamba kuhusu timu ya taifa anachojali ni uzalendo wa taifa lake.
    “Siwezi kusema lolote kuhusu kocha, mimi kama mchezaji naweza kucheza chini ya mwalimu yoyote, kwa timu ya taifa nasukumwa na uzalendo, huku (Mazembe) ni kazi,”amesema.
    Baada ya kupewa mikoba Stars, Nahodha huyo wa zamani wa Tanzania, Mkwasa aliteua wachezaji 26 wa kuingia kambini kwa ajili ya mchezo wa marudiano Raundi ya Kwanza kuwania tiketi ya kucheza michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) 2016 dhidi ya Uganda wiki ijayo mjini Kampala.
    Erasto Nyoni kulia hajaitwa katika kikosi cha Taifa Stars chini ya kocha mpya, Charles Boniface Mkwasa

    Na katika kikosi hicho aliwatema wachezaji kadhaa waliokuwamo kwenye kikosi cha Nooij, wakiwemo kipa Deo Munishi ‘Dida’ na mabeki Oscar Joshua na Erasto Nyoni. 
    Taifa Stars, inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager inaendelea na mazoezi Uwanja wa Boko Veterani, Dar es Salaam na imeweka kambi katika hoteli ya Kiromo mjini Bagamoyo.
    Wachezaji 26 waliopo kambini ni makipa; Mudathir Khamis (KMKM), Mwadini Ali (Azam FC) na Ally Mustafa ‘Barthez’ (Yanga) na mabeki ni Shomary Kapombe (Azam), Michael Aidan (Ruvu Shooting), Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ (Simba SC), Mwinyi Hajji Mngwali (KMKM), Nadir Haroub ‘Cannavaro’ (Yanga SC), Kevin Yondan (Yanga SC), Hassan Isihaka (Simba SC)na Andrew Vincent (Mtibwa Sugar).
    Viungo ni Mudathir Yahya (Azam FC), Abdi Banda (Simba SC), Salum Telelea (Yanga SC), Frank Domayo (Azam FC), Simon Msuva (Yanga SC), Said Ndemla (Simba SC), Ramadhani Singano ‘Messi’ (Simba SC) na Deus Kaseke (Mbeya City).
    Washambuliaji ni John Bocco (Azam FC), Atupele Green (Kagera Sugar), Rashid Mandawa (Kagera Sugar), Ame Ali (Mtibwa Sugar), wakati wengine ambao wamewekwa akiba ni Juma Abdul wa Yanga SC na Samuel Kamuntu wa JKT Ruvu.
    Mara baada ya kuteuliwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kurithi mikoba ya Mholanzi, Mart Nooij aliyefukuzwa mwishoni mwa wiki kufuataia kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Uganda katika mchezo wa kwanza na Uganda, Mkwasa alitaja benchi lake Ufundi, akimteua King Kibaden kuwa Mshauri wake wa Ufundi.
    Hemed Morocco kocha Msaidizi, Manyika Peter kocha wa makipa, Mtunza Vifaa ni Hussein Swedi ‘Gaga’, Meneja Juma Mgunda na Mratibu Msafiri Mgoyi, wakati Daktari atatajwa baadaye.
    Stars itaendelea kuwa kambini Kiromo na kufanya mazoezi Boko Veterani hadi itakaposafiri kwenda Uganda ambako inatakiwa kushinda 4-0 ili kusonga mbele CHAN.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ULIMWENGU: SIKUFIKIRIA ERASTO NYONI ANGEACHWA TAIFA STARS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top