![]() |
| Milovan, kocha wa Simba |
WAKATI homa ya pambano la kimataifa kati ya Simba na Es
Setif ya Algeria ikizidi kupamba moto, kocha mkuu wa wekundu hao Mserbia
Curkovic Milovan amewataka mabeki wake Juma Nyoso na Kelvin Yondan na Amir
Maftah kuwa makini zaidi kwani wana kazi kubwa ya kuzuia mipira ya juu na kona
ambayo imekua ikitumiwa sana na wapinzani wao. Milovan ambaye katika mazoezi ya juzi alionekana zaidi
akiwapa mbinu mabeki hao kwa kuwafundisha jinsi ya kupambana na mipira ya juu
pamoja na kona, amewataka kuongeza umakini katika eneo lao. Katika mazoezi hayo, Milovan aliwatumia Uhuru Seleman na
Salum Machaku kupiga mipira ya kona ili kuwapa uzoefu mabeki jinsi ya kucheza
na kuokoa mipira hiyo. "Tumejiandaa vizuri na wachezaji wote wako katika hali
nzuri, kiufundi timu ipo katika kiwango cha kuridhisha ingawa nilikua nikiwapa
mbinu zaidi mabeki ambao naamini wana kazi kubwa," alisema Milovan. Aidha kwa upande wa washambuliaji Okwi, Mafisango na Felix
Sunzu nao walikua wakipewa kazi ya ziada ya kuhakikisha wanamiliki mipira na kufunga
mabao ya haraka. Akizungumza hali ya Juma Jabu ambaye ni majeruhi, alisema
huenda nafasi yake ikachezwa na Amir Maftah ambaye naye jana alikuwa akipatiwa
mazoezi ya aina yake. Wakati Milovan akiwapa wachezaji wake mbinu hizo, kocha wa
Setif, Geiger Alain kwenye mazoezi ya timu yake Uwanja wa Karume alikuwa
akiweka mkazo washambuliaji wake kufunga mabao mengi. Milovan atalazimika kutafuta mbinu bora haraka ili kuzuia
mashambulizi ya hatari ya kipindi cha pili kutoka kwa ES Setif kwa ajili ya
kujihakikisha matokeo mazuri. Udhaifu mkubwa Simba msimu huu upo katika kipindi cha pili,
ambapo wanaonekana kuchoka na kuruhusu mashambulizi mengi langoni mwao jambo
lililofanya mpaka sasa kufungwa mabao 9 kati ya 14 katika muda huo. Rekodi hiyo mbaya ya kiuchezaji iliyoonyeshwa na Simba msimu
huu itakuwa ni faida kubwa kwa wapinzani wao ES Setif waliojijengea utamadumi
wa kupata ushindi katika kipindi cha pili. Simba walifika fainali katika mashindano ya Kombe la
Shirikisho la Soka Afrika mwaka 1993, ambapo ilicheza mechi ya kwanza na Stella
Club na kutoka suluhu 0-0 nchini Ivory Coast na zilirudiana nchini Tanzani,
timu ya Simba ilifungwa 2-0 na Stella kutwaa ubingwa.



.png)
0 comments:
Post a Comment