• HABARI MPYA

    Saturday, March 24, 2012

    HUYU NDIYE KHADIJA OMAR ABDALLAH KOPA

    Khadija Omar Abdallah Kopa, gwiji wa Taarab
    ANTHONY NYONGESA
    IWAPO unadhani kwamba muziki wa kizazi kipya, Hip Hop, ndiyo unaopendwa pekee basi wajidanganya.
    Subiri wakati tamasha la taarab litakapoandaliwa jijini ndipo utaona idadi ya mashabiki kuanzia kwa vijana hadi kwa watu wazima wanavyoshabikia taarab.
    Licha ya kuhusishwa awali na wakazi wa Pwani, muziki wa taarab umeibuka kuwa maarufu mno jijini Nairobi katika miaka ya sasa.
    Unapotaja taarab, basi mtaje pia mama wa sauti ya chiriku ambaye mashairi yake huwaacha mashabiki wakiweweseka.
    Huyu ni Malkia wa Mipasho kwa nyimbo zake za kuwapa vidonge vyao ni Bi. Khadija Omar Abdallah, maarufu kama Khadija Kopa ambaye kila anapotangaza kuandaa shoo jijini Nairobi, tiketi huuzwa na kukwisha kabla ya siku ya tamasha.
    Kwa wasiomjua, yeye hahitaji kutambulishwa kwani ndiye aliyeviporomosha vibao kadhaa ikiwa ni pamoja na Y2K, Utaishia Kunawa, Top In Town, Full Stop, Full Kujiachilia, Gendaeka, Mambo Iko Huku, Nalijua Jiji, miongoni mwa zingine nyingi.
    Iwapo huvishiki vibao basi basi tafuta kanda zake au kuvikia kwenye mtandao ili ujionee wewe mwenyewe.
    Alipokuwa na shoo yake jijini Nairobi miezi mitatu iliyopita, mama huyu alizungumza na Mwanaspoti kuhusu masuala mbalimbali kuanzia muziki na maisha yake.
    Shoo yake ilivutia mno na mashabiki wa umri wa makamo ambao si kawaida kwao kufika katika tamasha linalodhaniwa kuwa ni la wakongwe hasa wale wa Pwani.
    Mwimbaji huyu mwenye jina kubwa Afrika Mashariki, analalamikia kuhusu ukosefu wa sapoti ya kutosha kutoka kwa mashabiki ambao kwa kawaida wanapenda kununua kanda gushi- zile zilizonaswa na walanguzi na badala yake kuwacha zile halali za wasanii.
    Tunatengeneza nyimbo zetu halafu sisi wenyewe hatufaidiki. Watu wanaingilia kazi zetu. Kwa mfano mimi nimeanza kuimba muda mrefu sasa. Lakini bado kazi zangu haziniletei faida, alisema.
    Khadija Kopa anasema alizaliwa mwaka 1963 kisiwani Zanzibar na ni mtoto wa kipekee katika familia ya Kopa. Nimeolewa na nina watoto wanne na wajukuu wawili. Kwa bahati mbaya, mwanangu mmoja, Omar Kopa, alifariki miaka michache iliyopita, alisema kuhusu Omar ambaye pia alikuwa mwimbaji wa kutajika mno.
    Omar alivuma na bendi ya Tanzania One Theatre (TOT) pia ya Tanzania kwa nyimbo zake kama vile Nipepee, Nifagilieni na Tuko Benet.
    Kopa sasa amebakiwa na watoto wawili wa kiume mmoja wa kike.
    Mbali ya muziki, Kopa ni mama wa nyumbani, mfanyabiashara na pia mwanaharakati wa kisiasa kwao nyumbani Tanzania.
    Mama huyu alipata sifa zaidi kutokana na uimbaji. Lakini si wengi wanaojua kuwa ni kipawa alichozaliwa nacho.
    Anasema kuwa alikuwa akipenda kuimba tangu akiwa mdogo, akisomea madrasa Zanzibar.
    Nikiwa chuoni (madrasa) nilikuwa msomaji mzuri wa qaswida, halafu vilevile nilipokuwa Young Pioneer, nilikuwa kwenye kikundi cha kwaya, anasema.
    Shuleni vilevile nilikuwa kwenye mambo ya ngoma, mambo ya utamaduni na kwaya. Shule yetu ilikuwa ni bingwa kwa kwaya Zanzibar. Niliendelea hivyo hadi katika shule ya upili.
    Siku moja nilikuwa nimekaa nikiiga wimbo. Akapita babu yangu aliye katika kikundi cha Culture Musical Club cha Zanzibar. Akaniambia najua kuimba. Basi akachukua hatua ya kuniandikia barua mwenyewe bila kunishauri, akaipeleka Culture Musical Club kuomba nijiunge nao.
    Akishirikiana na waimbaji wengine wa kike kama vile Mwanamtama Amir, marehemu Leila Khatib na wanaume kama Abdul Misambano na Ali Star, waliporomosha nyimbo ambazo zitasalia milele masikioni mwa wapenzi wa taarab.
    Kwa miaka zaidi ya 11 sasa, Kopa ameendelea kuporomosha muziki na sauti yake ile ile isiyokwisha utamu.
    Anasema kinyume na uvumi kuwa kundi la TOT Taarab limesambaratika, lipo na linaendelea kuwaongoa wapenzi wake.
    Halijasambaratika. TOT ni kikundi kikubwa kinachokuwa katika shughuli nyingi zikiwemo siasa wakati mwingine, alifichua mama.
    Mwimbaji huyu wa kusifika, anasema ana mipango ya kutoa albamu yake ya kibinafsi na tayari wimbo wake Mji ni Chuo Kikuu unachezwa na vituo vingi vye redio.
    Katika TOT tumetoa albamu hivi juzi juzi. Hii yaitwa Fullstop. Tunajitayarisha kufanya mkanda wa video. Lakini mimi mwenyewe nataka kutoa albamu yangu Mji ni Chuo Kikuu. Itakuwa na nyimbo nne ambazo baadhi nimewashirikisha Fatma Issa na Saada Mohamed, anasema.
    Anawataka wapenzi wa muziki wasiwe wepesi wa kutaka kusikiza nyimbo zilizotengezwa vichochoroni na watu wasiowajali waimbaji.
    Kwa wapenzi wangu, mimi nawapenda na wao wanipende tu wasijaliWapende muziki wa taarab watuinue sisi wasanii wao, anasisitiza.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HUYU NDIYE KHADIJA OMAR ABDALLAH KOPA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top