• HABARI MPYA

  Thursday, January 03, 2019

  AZAM FC YAANZA NA SARE KOMBE LA MAPINDUZI, 1-1 NA JAMHURI AMAAN

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MABINGWA watetezi, Azam FC wamefungua pazia la michuano ya Kombe la Mapinduzi mwaka 2019 kwa kutoka sare bao 1-1 dhidi ya Jamhuri, mchezo uliofanyika Uwanja wa Amaan, Zanzibar usiku wa Jumanne.
  Sare hiyo ya Azam FC iliyoko Kundi B la michuano hiyo, inaifanya kujikusanyia pointi moja, ikiwa kileleni mwa msimamo sambamba na Jamhuri zilizolingana kila kitu, huku Malindi na KVZ zikifuatia ambazo nazo zilitoka suluhu kwenye mechi yao ya awali iliyopigwa Jumanne.
  Yanga pekee ndiyo haijacheza mechi katika kundi hilo ikitarajia kukipiga KVZ Alhamisi.
  Mechi hiyo iliyokuwa na upinzani kwa pande zote mbili, ilishuhudiwa Azam FC ikianza kuandika bao la uongozi dakika ya 28, lililofungwa na kiungo mshambuliaji, Tafadzwa Kutinyu, kwa mkwaju wa penalti uliotokana na Emmanuel Balele, kuunawa mpira wakati akiokoa shuti la mfungaji wa bao hilo.
  Jamhuri iliyocheza kwa nidhamu kubwa kwenye eneo la ulinzi hadi kufanikiwa kuwabana washambuliaji wa Azam FC, ilipata bao la kusawazisha dakika ya 66 lililofungwa na Abdul Ramadhan, bao lililowafanya kuambulia pointi hiyo moja.
  Matokeo hayo yanaifanya Azam FC kuhitaji matokeo mazuri kwenye mechi zake tatu zilizobakia za hatua ya makundi, ikianza na Yanga Jumamosi hii, mchezo unaofuatia utakaofanyika Uwanja wa Amaan saa 2.15 usiku.
  Kikosi cha Azam FC leo: Razak Abalora, Nickolas Wadada, Bruce Kangwa, Yakubu Mohammed, Agrey Moris (C), Stephan Kingue, Joseph Mahundi, Tafadzwa Kutinyu/Salmin Hoza dk 46, Donald Ngoma/Abadi Kawambwa dk 80, Obrey Chirwa, Enock Atta/Danny Lyanga dk 76.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AZAM FC YAANZA NA SARE KOMBE LA MAPINDUZI, 1-1 NA JAMHURI AMAAN Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top