• HABARI MPYA

    Saturday, January 19, 2019

    AHLY WACHOMOA DAKIKA YA 85 KUPATA SARE NA JS SAOURA

    MABINGWA wa kihistoria wa Afrika, Al Ahly usiku wa jana wamelazimisha sare ya kufungana bao 1-1 na wenyeji, JS Saoura Uwanja wa Agosti 20 1955 mjini Bechar katika mchezo wa Kundi D Ligi ya Mabingwa Afrika.
    Ahly sasa wanapanda kileleni mwa kundi hilo, wakifikisha pointi nne baada ya kucheza mechi mbili, wakifuatiwa na Simba yenye pointi tatu, JS Saoura pointi moja na AS Vita ambayo haina pointi inashika mkia.   
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Eric Arnaud Otogo-Castane aliyesaidiwa na Théophile Vinga na Boris Ditsoga wote wa Gabon, Sid Ali Yahia Cherif alianza kuwafungia wenyeji, JS Saoura dakika ya 59 akimalizia pasi ya Mohamed El Amine Hammia.
    Kikosi cha Al Ahly kilicholazimisha sare na JS Saoura jana nchini Algeria 

    Kikosi cha JS Saoura kilicholazimishwa sare na Al Ahly nyumbani jana

    Lakini makosa ya safu ya ulinzi ya JS Saoura yakaipa bao la kusawazisha Al Ahly dakika ya 85, mfungaji Karim Nedved akimalizia pasi ya Mohamed Hany.
    Kocha Mualgeria, Nabil Neghiz alimuinua mshambuliaji wake mpya, Mtanzania, Thomas Emmanuel Ulimwengu dakika ya 80 kwenda kuchukua nafasi ya Ziri Hammar.
    Kwa mara ya pili mfululizo, Ulimwengu akatumia vyema muda mfupi wa kucheza baada ya kutokea benchi kwa kuonyesha uwezo mkubwa kama ilivyokuwa kwenye mechi dhidi ya Simba Dar es Salaam Saoura wakichapwa 3-0.
    Mechi nyingine ya Kundi D inafuatia leo, AS Vita waliochapwa 2-0 na Al Ahly kwenye mechi ya kwanza wiki iliyopita Misri wanawakaribisha Simba SC mjini Kinshasa Saa 1:00 usiku.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AHLY WACHOMOA DAKIKA YA 85 KUPATA SARE NA JS SAOURA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top