• HABARI MPYA

  Wednesday, January 02, 2019

  AMRI SAID ‘STAM’ AANZA VYEMA BIASHARA UNITED, YAICHAPA MEYA CITY 2-1

  Na Mwandishi Wetu, MUSOMA
  KOCHA mpya, Amri Said ‘Stam’ ameanza vyema Biashara United baada ya kuiongoza timu hiyo kuibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Mbeya City Uwanja wa Karume mjini Musoma mkoani Mara.
  Ushindi huo wa kwanza tu wa kocha Amri Said tangu ajiunge na timu hiyo juzi akitokea kwa majirani, Mbao FC ya Mwanza umetokana na mabao ya Daniel Manyenye dakika ya 18 na Juma Mpakala dakika ya 20, wakati bao la Mbeya City limefungwa na Frank Ikobela dakika ya 26.
  Biashara United iliyopanda Ligi Kuu msimu huu, inafikisha pointi 13 katika mechi ya 18 baada ya ushindi huo, ikipanda kwa nafasi moja hadi ya 19 ikiiteremshia mkiani Tanzania Prisons, nafasi ya 20.
  Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Alliance FC imeutumia vyema Uwanja wa nyumbani, Nyamagana mjini Mwanza baada ya kuibuka na ushindi wa 3-0 Ruvu Shooting. 
  Mabao ya Alliance FC yamefungwa na Hussein Javu dakika ya 12, Dickson Ambundo dakika ya 24 na Bigirimana Blaise dakika ya 32.
  Na Uwanja wa Samora mjini Iringa, bao pekee la Jimmy Shoji dakika ya 64 limeipa ushindi wa 1-0 Lipuli FC dhidi ya Tanzania Prisons.
  Nayo Stand United imeibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya JKT Tanzania bao pekee la Morice Mahela dakika ya 73 Uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga, wakati Kagera Sugar imelazimishea sare ya 0-0 na jirani zao, Mbao FC ya Mwanza Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
  Wenyeji, Singida United wamelazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na Coastal Union katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu leo Uwanja wa Namfua mjini Singida. Mbwana Hamisi ‘Kibacha’ alianza kuifungia Coastal Union dakika ya 58, kabla ya Geofrey Mwashiuya kuisawazishia Singida United dakika ya 63.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AMRI SAID ‘STAM’ AANZA VYEMA BIASHARA UNITED, YAICHAPA MEYA CITY 2-1 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top