• HABARI MPYA

    Friday, January 18, 2019

    NSAJIGWA, MWASHIUYA WAFUNGIWA NA KUPIGWA FAINI YA SH. 500,000 KILA MTU

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KOCHA Msaidizi wa timu ya Singida United, Nsajigwa Shadrack Joel Mwandemele amefungiwa mechi mbili na kutozwa faini ya Sh. 500,000 kwa kosa la kupinga maamuzi ya refa kwenye mechi dhidi ya Stand United Desemba 7, mwaka jana Uwanja wa Namfua mjini Singida.
    Maamuzi hayo yamefikiwa katika kikao cha Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji wa Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kamati ya Saa 72 kilichofanyika hivi karibuni mjini Dar es Salaam. 
    Afisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Clifford Mario Ndimbo amesema leo katika taarifa yake kwamba katika mchezo huo ambao Singida United walichapwa 1-0, Nsajigwa amefungiwa baada ya kuondolewa kwenye benchi la ufundi kwa kosa la kumpinga maamuzi.
    Ndimbo amesema kwamba adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 41(11) ya Ligi Kuu Toleo la 2018 kuhusu Udhibiti kwa Makocha.
    Nsajigwa Shadrack (kushoto) amefungiwa mechi mbili na kutozwa faini ya Sh. 500,000 

    Naye kiungo mshambuliaji wa Singida United, Godfrey Mwashiuya amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya Sh. 500,000 baada ya kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumpiga mpinzani wake ngumi kwa makusudi wakati mpira ukiwa umesimama.
    Mwashiuya, mchezaji wa zamani wa Yanga, anadaiwa kufanya kosa hilo katika mechi dhidi ya wenyeji, Biashara United Januari 6, mwaka huu Uwanja wa Karume, Musoma mkoani Mara timu hizo zikitoka sare ya bila kufungana.
    Mchezaji mwenzake wa Singida Utd, Rajab Zahir amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya Sh. 500,000 baada ya kutolewa kwa kadi nyekundu kwenye mchezo huo kufuatia kumtolea lugha chafu refa na kutaka kumpiga baada ya mchezo kumalizika. 
    Na Ndimbo amesema wote wawili adhabu zao zimezingatia kanuni ya 38 (9) ya Ligi Kuu Toleo la 2018 kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.
    Singida United yenyewe imetozwa faini ya Sh. 200,000 kwa kutoingia kwenye chumba cha kubadilishia nguo kwenye mechi dhidi ya Simba Desemba 30, mwaka jana.
    Singida United ambayo ilifungwa 3-0 kwenye mchezo huo, ilikwenda kubadilishia nguo kwenye chumba cha waandishi wa habari, jambo lililosababisha usumbufu kwa waandishi wa habari na adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu Toleo la 2018 kuhusu Taratibu za Mchezo.
    Mechi namba 165- Desemba 15, 2018: Ndanda 1 vs African Lyon 0. Kocha wa makipa wa African Lyon, Juma Bomba amefungiwa mechi mbili na kupigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) baada ya kuondolewa kwenye benchi la ufundi kwa kosa la kupinga maamuzi ya Mwamuzi. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 41(11) ya Ligi Kuu Toleo la 2018 kuhusu Udhibiti kwa Makocha.
    Mechi namba 167- Desemba 16, 2018: Yanga 3 vs Ruvu Shooting 2. Mtunza Vifaa wa Ruvu Shooting, Augustine Palangwa anapelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa kosa la kutoa lugha ya matusi kwa Waamuzi.
    Mechi namba 192-Januari 5, 2019: Mbao 0 vs Alliance FC 0. Klabu za Mbao na Alliance FC zimepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kila moja kwa kushindwa kuingiza timu za U20 kwenye mechi ya utangulizi. Faini hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 71(2)(a) ya Ligi Kuu Toleo la 2018 kuhusu Vijana na Watoto.
    Pia Alliance FC imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa kutoingia kwenye vyumba vya kubadilishia, hivyo kufanya timu yao ikaguliwe nje ya vyumba. Adhabu hiyo imezingatia Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu Toleo la 2018 kuhusu Taratibu za Mchezo.
    Mechi namba 124- Novemba 3, 2018: JKT Tanzania 0 vs Simba 2. Mwamuzi Msaidizi namba mbili Mashaka Mwandembwa amefungiwa miezi mitatu kwa kushindwa kutafsiri vizuri sheria ya kuotea. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 39 ya Ligi Kuu Toleo la 2018 kuhusu Udhibiti kwa Waamuzi. Pia Mwamuzi Mbaraka Rashid amepewa Onyo kwa kutokuwa makini wakati wa akichezesha mechi hiyo.
    Mechi namba 50- Januari 13, 2019: Pamba 4 vs Green Warriors 2. Klabu ya Green Warriors imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na mshabiki wa timu yao kufanya vitendo vinavyoashiria imani za ushirikina. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 43(1) ya Ligi Daraja la Kwanza Toleo la 2018 kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
    Pia klabu hiyo imetozwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na baadhi ya washabiki wao wakiongozwa na benchi la ufundi kuwazonga waamuzi huku wakiwatolea lugha chafu na kutaka kuwapiga baada ya mchezo kumalizika. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 43(1) ya Ligi Daraja la Kwanza Toleo la 2018 kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
    Mechi namba 59- Januari 13, 2019: Mgambo Shooting 0 vs Geita Gold 1. Klabu ya Mgambo Shooting imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na washabiki wake kuwa ndani ya uzio unaotenganisha wachezaji na washabiki kwa muda wote wa mchezo, licha ya kutakiwa kuondoka. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 43(1) ya Ligi Daraja la Kwanza Toleo la 2018 kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
    Mchezaji wa Mgambo Shooting, Dunstan D. Lipinga (jezi namba 30) anapelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa kumpiga Mwamuzi baada ya mchezo kumalizika. Pia mchezaji Rashid A. Shilla wa Mgambo (jezi namba 19) anapelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF baada ya kumpiga Meneja wa Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi.
    Mechi namba 17- Novemba 18, 2018: Mtwivila 0 vs The Mighty Elephant 0. Klabu ya The Mighty Elephant imepewa Onyo Kali kwa kutohudhuria kikao cha maandalizi ya mchezo (technical meeting) bila kutoa taarifa yoyote kwa Kamishna. Adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(3) ya Ligi Daraja la Pili Toleo la 2018 kuhusu Taratibu za Mchezo.
    Pia The Mighty Elephant imepigwa faini ya sh. 200,000 (laki mbili) kwa kuchelewa kufika uwanjani kwa dakika 20. Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 14(48) ya Ligi Daraja la Pili kuhusu Utaratibu wa Mchezo.
    Mechi namba 18- Novemba 18, 2018: Kitayosce 0 vs Kilimanjaro Heroes 0. Kocha wa Kitayosce, Hamad Haule amefungiwa mechi mbili na kupigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) baada ya kuondolewa kwenye benchi kwa kosa la kuongea na simu hata baada ya kukatazwa na Mwamuzi wa Akiba. Adhabu imezingatia Kanuni ya 41(11) ya Ligi Daraja la Pili Toleo la 2018 kuhusu Udhibiti kwa Makocha.
    Pia Mtunza Vifaa wa Kilimanjaro Heroes, Noel Paul anapelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF baada ya kuondolewa kwenye benchi kwa kosa la kuongea na simu, licha ya kukanywa asitumie simu lakini alikaidi.
    Mechi namba 27- Januari 5, 2019: Kitayosce 1 vs Mtwivila 1. Kocha wa Mtwivila, Lisa Mwalupindi amefungiwa mechi mbili na kupigwa faini ya sh. 300,000 (laki tatu) baada ya kuondolewa kwenye benchi kwa kupinga mwamuzi ya Mwamuzi. Adhabu imezingatia Kanuni ya 41(11) ya Ligi Daraja la Pili Toleo la 2018 kuhusu Udhibiti kwa Makocha.
    Naye Daktari wa Kitayosce, Michael Evarest anapelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF baada ya kutolewa kwenye benchi la ufundi kwa kosa la kuchelewesha kuanzishwa kwa mchezo baada ya kuamriwa na Mwamuzi atokee sehemu ya karibu alikaidi na kutokea sehemu ya mbali.
    Mechi namba 18- Novemba 17, 2018: Bulyanhulu 0 vs Kasulu Red Star 0. Meneja wa Kasulu Red Star, Kapama Kapama anapelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa kutoa lugha ya matusi kwa Mwamuzi.
    Mechi namba 28- Januari 6, 2019: Milambo vs Madini SC. Timu ya Madini SC imeshushwa madaraja mawili kwa kutofika uwanjani. Hivyo, matokeo ya mechi zote ilizocheza yamefutwa ili kutoa uwiano sahihi kwa timu zilizobaki kwenye Ligi.
    Pia timu hiyo imepigwa faini ya sh. 2,000,000 (milioni mbili). Adhabu hizo zimetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 28 (1) na (2) ya Ligi Daraja la Pili Toleo la 2018 kuhusu Kutofika Uwanjani.
    Mechi namba 25- Januari 5, 2019: Cosmopolitan 1 vs Changanyikeni 0. Klabu ya Changanyikeni imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kutokana na washabiki wa timu yao kumpiga Mwamuzi huku wakimtolea lugha ya matusi. Adhabu imezingatia Kanuni ya 43(1) ya Ligi Daraja la Pili Toleo la 2018 kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
    Mmiliki wa timu ya Changanyikeni, Omar Bawazir anapelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF baada ya kuingia uwanjani na baadhi ya washabiki na kumpiga Mwamuzi.
    Vilevile Mwamuzi wa mechi hiyo, Ibrahim Mohamed ameondolewa kwenye Orodha ya Waamuzi wa SDL baada ya kupata alama za chini.
    Mechi namba 27- Januari 6, 2019: African Sports 0 vs Forest 2. Malalamiko ya African Sports kuwa usajili wa wachezaji Timotheo Emmanuel Kombo na Lawrence Milton Mganga wa Forest si halali yamekataliwa. TFF imethibitisha kuwa wachezaji hao wamesajiliwa kihalali kwenye timu ya Forest.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NSAJIGWA, MWASHIUYA WAFUNGIWA NA KUPIGWA FAINI YA SH. 500,000 KILA MTU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top