• HABARI MPYA

  Tuesday, January 01, 2019

  AZAM FC KUANZA KUTETEA KOMBE LA MAPINDUZI KESHO ZANZIBAR

  Na Mwandishi Wetu, ZANZIBAR
  MABINGWA watetezi wa michuano ya Kombe la Mapinduzi, Azam FC kesho wanatarajia kufungua pazia la michuano hiyo kwa kuvaana na Jamhuri ya Pemba, mchezo utakaofanyika Uwanja Amaan, Zanzibar kuanzia Saa 2:15 usiku.
  Kikosi cha Azam FC kilichotwaa ubingwa wa michuano hiyo mara mbili mfululizo, kipo kwenye hali nzuri kabisa na leo asubuhi kilifanya mazoezi ya mwisho kwenye Uwanja wa Dimani, tayari kujiweka sawa na mtanange huo unaotarajia kuwa mkali.
  Kocha Mkuu wa Azam FC, Mholanzi Hans Van Der Pluijm amesema kwamba wanaingia na malengo ya kujaribu kutwaa taji hilo na kuendeleza rekodi nzuri waliyokuwa nayo kwenye ushiriki wao kila mwaka.
  Kocha Mkuu wa Azam FC, Hans Van Der Pluijm (kulia) akiwa na Msaidizi wake, Juma Mwambusi 
  Washambuliaji wa Azam FC, Obrey Chirwa na Donald Ngoma wakati timu ikiwaili Zanzibar jana

  “Unapoenda kwenye michuano, hauendi tu kwa lengo la kushiriki au kujaza idadi ya timu, tunataka kushinda taji, tunapaswa kufanya hivyo kama tunavyofanya katika ligi mechi hadi mechi, tunajiandaa kila wakati hasa kujenga saikolojia na akili, hili ni jambo la muhimu sana kwa wachezaji wa Kitanzania,” alisema.
  Huo utakuwa ni mchezo wa pili mfululizo kwa timu hizo kukutana, mara ya mwisho kukutana ni kwenye michuano iliyopita na Azam FC kuichapa mabao 4-0, yaliyowekwa kimiani na mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo, Bernard Arthur, kiungo Salmin Hoza, Yahya Zayed na Paul Peter.
  Aidha timu hizo pia ziliwahi kukutana kwenye mchezo wa fainali ya michuano hiyo mwaka 2012, na Azam FC kuandika rekodi ya kutwaa taji la kwanza kati ya manne ya Kombe la Mapinduzi, ikishinda mabao 3-1, yaliyofungwa na gwiji wa timu hiyo, John Bocco ‘Adebayor’, Mrisho Ngassa na Mrisho Ahmed aliyejifunga.
  Azam FC ipo Kundi B la michuano hiyo, sambamba na timu nyingine za Yanga, Jamhuri, KVZ na Malindi.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AZAM FC KUANZA KUTETEA KOMBE LA MAPINDUZI KESHO ZANZIBAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top