• HABARI MPYA

    Wednesday, September 20, 2017

    SIMBA TAYARI KWA SHUGHULI NA MBAO FC KESHO KIRUMBA

    Na Princess Asia, MWANZA
    KIKOSI cha Simba asubuhi ya leo kimefanya mazoezi yake ya mwisho kuelekea mchezo wake wa kesho wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya wenyeji, Mbao FC Alhamisi Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
    Kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog aliteremka Uwanja wa CCM Kirumba  na vijana wake kwa mazoezi ya takriban saa mbili kujiandaa na mchezo huo unaotarajiwa kuwa mkali na wa kusisimua.
    Simba inataka kuendeleza ubabe wake kwa Mbao FC baada ya msimu uliopita kushinda mechi zote tatu walizokutana, zikiwemo mbili za Ligi Kuu msimu uliopita Alhamisi ya Oktoba 20 iliposhinda 1-0 Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na Jumatatu ya Aprili 10 iliposhindaa 3-2 Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
    Wachezaji wa Simba leo Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza leo

    Mchezo mwingine ulikuwa wa fainali ya Kombe la Azam Sports Federation Cup Mei 27, mwaka huu ambao Simba walishinda 2-1 ndani ya dakika 120 Uwanja wa Jamhuri Dodoma.
    Tayari Simba SC imecheza mechi tatu za Ligi Kuu msimu huu, ikishinda mbili 7-0 dhidi ya Ruvu Shooting na 3-0 dhidi ya Mwadui FC Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, wakati mwingine wametoka sare ta 0-0 na Azam Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
    Katika mabao 10 iliyovuna kwenye mechi mbili, mshambuliaji Mganda, Emmanuel Okwi amefunga mabao sita, manne dhidi ya Ruvu na mawili dhidi ya Mwadui, sasa akiwa anaongoza kwa kufunga katika Ligi Kuu.  
    Ligi Kuu itaendelea Jumamosi baada ya kesho, mabingwa watetezi, Yanga watacheza na Ndanda FC ya Mtwara kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, Singida United itaialika Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma wakati Tanzania Prisons itakuwa mgeni wa Mwadui ya Shinyanga katika mchezo utaofanyika Uwanja wa Mwadui ilihali Majimaji itakuwa mwenyeji wa Njombe Mji kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea.
    Jumapili kutakuwa na michezo mitatu ambako Ruvu Shooting itaialika Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani huku Stand United ikicheza na Mbeya City kwenye Uwanja wa Kambarage mkoani Shinyanga.
    Wakati mechi zote hizo hapo juu zikianza saa 10.00 jioni, mchezo mwingine siku ya Jumapili utaanza saa 1.00 jioni kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi ukikutanisha Azam na Lipuli ya Iringa.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA TAYARI KWA SHUGHULI NA MBAO FC KESHO KIRUMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top