• HABARI MPYA

    Thursday, February 28, 2013

    TEGETE ANAKOSA SANA, KAVUMBANGU HADI PENALTI INAOATA MBAWA!

    Tegete akirejea uwanjani kinyonge
    baada ya kukosa bao la wazi

    Na Mahmoud Zubeiry
    KATIKA mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima, amekuwa lulu kwa klabu yake, Yanga SC kutokana na kuifungia mabao muhimu ya ushindi.
    Jumamosi iliyopita, Nahodha huyo wa Rwanda, alifunga bao pekee la ushindi katika mchezo dhidi ya Azam FC, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam tena kwa juhudi binafsi.
    Baada ya kupiga krosi za kutosha na pasi ze kupenyeza kwenye njia huku washambuliaji wa timu hiyo wakishindwa kuziunganisha nyavuni, Niyo aliamua kufanya juhudi za kuipa ushindi timu yake.
    Aliwatoka wachezaji wa Azam kwa chenga za kutishia anakwenda huku, kumbe anakwenda kule, na walipodanganyika akamtazama kipa Mwadini Ally amekaaje langoni na kufumua shuti lililotinga nyavuni.
    Hilo lilikuwa bao muhimu sana kwa Yanga, kwani liliifanya timu hiyo ifikishe pointi 39 na kuwaacha Azam, ambao kwa sasa ndio wapinzani wao wakuu kwenye mbio za ubingwa kwa pointi tatu.
    Siku hiyo, washambuliaji wote wa Yanga, Jerry Tegete, Hamisi Kiiza na Didier Kavumbangu walikosa mabao kadhaa ya wazi. Tegete ndio zaidi, siku hiyo alishindwa kufunga katika nafasi tatu nzuri.
    Baada ya mechi hiyo, mashabiki walimponda sana mshambuliaji huyo, ambaye husifiwa anajua kufunga na katika mechi iliyofuata, jana kocha Mholanzi, Ernie Brandts alimuanzishia benchi Tegete.
    Didier Kavumbangu akaanza pamoja na Said Bahanuzi, lakini nao pia hawakufanikiwa kufunga. Wote walipambana sana, lakini walipofika kwenye eneo la hatari la wapinzani, kufunga lilikuwa suala gumu.
    Kavumbangu aliingia kwenye eneo la hatari la Kagera mwishoni mwa kipindi cha kwanza, akadakwa miguu na kipa Hannington Kalyesebula, refa akaamuru ipigwe penalti.
    Kavumbangu akikosa bao la wazi. Alikosa na penalti pia jana.
    Kavumbangu kwa sasa ndiye mtaalamu wa kupiga penalti Yanga, lakini akaenda kupiga juu ya lango. Kipindi cha pili, walitolewa wote Bahanuzi na Kavumbangu wakaingizwa Tegete na Kiiza, lakini nao walipambana sana, ila kufunga ilikuwa zoezi gumu kwao pia.
    Hatimaye kwa mara nyingine tena katika mechi ya pili mfululizo, jana Niyonzima akarudia kufunga kwa aina ile ile aliyofunga kwenye mechi na Azam na likawa bao lenye uzito ule ule, wa pointi tatu.       
    Mabingwa watetezi, Simba SC wanashika nafasi ya tatu kwa sasa kwenye Ligi Kuu kwa pointi zao 31, wakiwa  nyuma ya Azam yenye pointi 36 na Yanga 42 waliopo kileleni.
    Simba SC wameuweka rehani ubingwa wao wa Ligi Kuu na hata kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, pia wanachungulia mlango wa kutokea, hiyo inafuatia kufungwa 1-0 na Recereativo de Libolo ya Angola nyumbani katika mchezo wa kwanza wa Raundi ya Kwanza wiki iliyopita.
    Sasa Simba SC wanatakiwa kushinda 2-0 wasonge mbele, kazi wanayo. Sababu kubwa ya Simba kuelekea kutema ubingwa wa Bara, na pia kutolewa mapema katika Ligi ya Mabingwa inaelezwa ni kukosa washambuliaji.
    Niyonzima akipoza koo baada ya kuifungia Yanga dhidi ya Azam
    ‘Wataalamu’ wanasema timu haina washambuliaji, lakini ukienda kwa wapinzani wao wa jadi, wana washambuliaji wanne, wote wazuri.
    Hata hivyo, ukifuatilia sana, washambuliaji wa Yanga wamekuwa wakifunga katika mechi nyepesi zaidi, ukiondoa Bahanuzi ambaye alifunga katika mechi ngumu kwenye Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
    Bahanuzi bado unaweza kuwa na matumaini naye, kwani ametoka kwenye majeruhi na anaanza taratibu na katika siku za karibuni, kasi yake inaonekana kuanza kurudi na bila shaka muda si mrefu, ataanza makeke yake tena.  
    Mbele ya mashabiki wa Yanga, tayari Tegete hawamtaki, lakini huyo Kavumbangu hadi penalti anakosa- Kiiza naye ndiyo hivyo tena, nani sasa anafaa? Swali gumu.
    Simba wanalia hawana washambuliaji wakati wana Abdallah Juma na Felix Sunzu, lakini wote wanawatoa kasoro. Bila shaka ipo haja ya kujifunza mbinu mbadala, kwani soka ni mchezo mpana sana siku hizi.
    Hispania walitufundisha kucheza bila mshambuliaji na wakachukua Kombe la Dunia mwaka 2010 Afrika Kusini- lakini pia, mabao rahisi yanaletwa na mfumo mzuri na mbinu nyingi pia.
    Ukitazama mpira wa Tanzania kwa sasa, staili ya kutafutia mabao ni kama moja tu, kwa mashambulizi ya kutokea pembeni. Kweli hiyo ni staili ambayo dunia nzima inatumika zaidi. Lakini haitoshi, lazima makocha wabangue bongo zao.
    Niyonzima akiwapigia makofi mashabiki baada ya mechi na Kagera jana
    Kweli wanakosa mabao ya wazi, wakiwa kwenye nafasi nzuri- na wanakosa wote, mbele ya wataalamu hilo si jambo la ajabu kwa mshambuliaji kushika kichwa akisikitika, au kushangilia baada ya kupiga mpira.
    Lakini kwa mashabiki wanapotaka ushindi, wanataka mshambuliaji ashangilie tu baada ya kupiga mpira, hii ni changamoto kwa makocha wa timu zetu, kuwa na mbinu mbadala kama Yanga sasa mara mbili mfululizo Niyonzima ameibeba timu.
    Hata beki, anaweza kuandaliwa katika mbinu ya kufunga, inapotokea washambuliaji ‘hawajaamka vizuri’. Ndiyo mambo ya soka hayo, Barcelona inafungwa 3-1 na Lionel Messi yuko uwanjani, ajabu gani kwetu hapa washambuliaji wetu kushindwa kufunga?
    Inakera sana mashabiki kuzomea wachezaji na hawajui athari yake, ni kwamba wanawaondoa mchezoni wachezaji na wanawavunjia hali ya kujiamini, hivyo kujikuta wanaharibu zaidi.
    Mfano ni Abdallaha Juma wa Simba, siku za mwanzoni alipokuwa anaingia katika timu hiyo, alikuwa anacheza vizuri na kufunga, lakini alipoanza kukosea kidogo tu, akawa anazomewa na mashabiki wakawa hawamtaki uwanjani.
    Hali hiyo imemfanya sasa Abdallah apoteze kujiamini na kujikuta anaharibu zaidi, kiasi kwamba hana msaada tena kwenye timu. 
    Soka ni mchezo mpana sana na una mambo mengi na ni vigumu kubadilisha hisia za mashabiki, lakini tujiulize, kama Tegete hafungi na Kavumbangu anakosa hadi penalti, nani afadhali? 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: TEGETE ANAKOSA SANA, KAVUMBANGU HADI PENALTI INAOATA MBAWA! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top