• HABARI MPYA

    Wednesday, February 20, 2013

    SIMBA YAZINDUKA, AZAM YAIPUMULIA YANGA KWA FUJO

    Mcha Vialli; Mfungaji wa mabao mawili ya Azam leo

    Na Prince Akbar
    AZAM FC imezidi kuitia presha Yanga kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kufuatia ushindi wa mabao 4-0 jioni ya leo dhidi ya JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
    Matokeo hayo yanaifanya Azam FC itimize pointi 36, baada ya kucheza mechi 17 pia, moja zaidi ya Yangana sasa ina mabao 31 ya kufunga na 14 ya kufungwa.
    Yanga inaendelea kuongoza msimamo wa Ligi Kuu, kwa wastani wake mzuri wa mabao, ingawa ina pointi sawa na Azam, 36, baada ya kucheza michezo 16, ikiwa imeshinda 11, imetoka sare tatu na kupoteza miwili, huku ikiwa imefunga jumla ya mabao 33 na kufungwa mabao 12 tu.
    Kocha wa Yanga, Mholanzi Ernie Brandts alikuwepo kwenye Uwanja wa Chamazi leo kuishuhudia Azam, ambayo watacheza nayo Jumamosi ikiendeleza dozi za ‘nne nne’, kwani na mechi iliyopita, Wana Lamba Lamba pia waliilaza Mtibwa Sugar 4-1.
    Hadi mapumziko, Azam walikuwa tayari mbele kwa mabao 2-0, yaliyotiwa kimaini na kiungo Khamis Mcha ‘Vialli’ na mshambuliaji John Bocco ‘Adebayor’.
    Mtoto wa Kizanzibari, Mcha ‘Vialli’ ndiye aliyefungulia biahsara Azam kwa bao lake la mapema dakika ya pili, akiunganisha krosi ya kiungo aliyerudishwa kwenye safu ya ulinzi, beki ya kulia Himid Mao. 
    JKT walipata nafasi ya kusawazisha bao dakika ya 10, baada ya kupata penalti, kufuatia kipa wa Azam, Mwadini Ally kumchezea rafu Samuel Kamuta, lakini mkwaju wa Kisimba Luambano ukapanguliwa na kipa huyo wa Lamba Lamba.
    Baada ya kosa hilo, Azam haikusita kuwaadhibu Maafande hao na alikuwa ni mshambuliaji tegemeo wa timu hiyo, John Raphael Bocco aliyefanya kazi hiyo dakika ya 44 na ushei, alipoifungia timu yake bao la pili akimalizia pasi ya kiungo Mkenya, Humphrey Mieno. 
    Kipindi cha pili, Azam walirudi na moto wao na kufanikiwa kupata mabao mawili zaidi.
    Mtoto wa Kizenji, Mcha Vialli alifungua tena biashara kipindi hicho mapema tu dakika ya kwanza ya kipindi hicho, akifunga kwa shuti kali, baada ya kupokea pasi maridadi ya Bocco Adebayor.
    Karamu ya mabao ya Azam leo hii ilihitimishwa na dakika ya 72 na kiungo Abdi Kassim Sadallah ‘Babbi’, aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Bocco Adebaor, ambaye alifunga bao la nne kwa shuti kali baada ya kupokea pasi ya Seif Abdallah, aliyeingia pia kipindi hicho kuchukua nafasi ya Kipre Tchetche.
    Katika mchezo huo, kikosi cha Azam kilikuwa; Mwadini Ali, Himid Mao, Waziri Salum, David Mwantika, Joackins Atudo, Jabir Aziz, Kipre Tchetche/Seif Abdallah dk 67, Ibrahim Mwaipopo/Gaudence Mwaikimba dk81, John Bocco ‘Adebayor’/Abdi Kassim ‘Babbi’ dk71, Humphrey Mieno na Khamis Mcha ‘Vialli’. 
    JKT Ruvu: Shaaban Dihile, Mussa Zuberi, Kessy Mapande, Kisimba Luambano/Hussein Dumba dk60, Damas Makwaya, Jimmy Shoji, Amos Mgisa/Emmanuel Pius dk 70, Nashon Naftal, Samuel Kamuta, Mussa Mgosi/William Sylvester dk60 na Hussein Bunu.
    Kiemba; Mfungaji wa bao la Simba SC leo
    Katika mechi nyingine za ligi hiyo, Simba SC leo ilizinduka baada ya sare mbili mfululizo na kufanikiwa kushinda 1-0 kwenyer Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, bao pekee la kiungo Amri Ramadhan Kiemba dakika ya 36. Kwa ushindi huo, Simba imefikisha pointi 31 baada ya kucheza mechi 17.
    Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga, Coastal Union imeibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya JKT Oljoro, mabao ya Suleiman Kassim ‘Selembe’ dakika ya 12 na Jerry Santo dakika ya 57, wakati Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, mabao ya Freddy Lewis dakika ya 26 na Benedict Mwamlagala dakika ya 89, yameipa African Lyon ushindi wa 2-0 dhidi ya wenyeji Toto African.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: SIMBA YAZINDUKA, AZAM YAIPUMULIA YANGA KWA FUJO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top