• HABARI MPYA

  Monday, January 14, 2019

  MBEYA CITY YAICHAPA MTIBWA 1-0 LEO SOKOINE NA KUIFIKIA KWA POINTI

  Na Mwandishi Wetu, MBEYA
  TIMU ya Mbeya City FC imeibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar FC katika mchezo wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara jioni ya leo Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
  Mchezo huo awali ulipangwa kufanyika jana, lakini ukaahirishwa hadi leo kutokana na mvua kubwa iliyonyesha kuharibu mandhari ya Uwanja.
  Bao pekee la Mbeya City inayofundishwa na kocha Mrundi, Ramadhani Nswazurimo limefungwa na mshambuliaji wake hodari, Eliud Ambokile kwa penalti dakika ya 83.
  Kwa matokeo hayo, Mbeya City inafikisha pointi 26 baada ya kucheza mechi 20 na kupanda hadi nafasi ya nane kutoka ya 12 katika ligi ya timu 20, wakati Mtibwa Sugar inabaki na pointi zake 26 baada ya kucheza mechi 17 na inaendelea kushika nafasi ya saba tu kwa wastani mzuri wa mabao.

  Ligi Kuu itaendelea kesho kwa mechi mbili Alliance FC ikiikaribisha Tanzania Prisons Uwanja wa Nyamagana mjini Mwanza na Yanga SC wakiwa wenyeji wa Mwadui FC Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Yanga SC ndiyo inaongoza Ligi Kuu kwa sasa ikiwa na pointi 50 baada ya kucheza mechi 18, ikiizidi kwa pointi 10 Azam FC katika nafasi ya pili ambayo imecheza mechi 17, wakati mabingwa watetezi, Simba SC ni wa tatu kwa pointi zao 33 za mechi 14 – na Mwadui FC yenye pointi 24 za mechi 21 ni ya 11. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MBEYA CITY YAICHAPA MTIBWA 1-0 LEO SOKOINE NA KUIFIKIA KWA POINTI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top