• HABARI MPYA

    Thursday, January 03, 2019

    MAREFA WA BOTSWANA KUCHEZESHA MECHI YA SIMBA NA JS SAOURA WIKI IJAYO DAR

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    MAREFA kutoka Botswana ndiyo watakaochezesha mechi ya kwanza ya Kundi D Ligi ya Mabingwa Afrika baina ya wenyeji Simba SC na JS Saoura ya Algeria Januari 12 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    Hao ni Joshua Bondo atakayepuliza kipyenga akisaidiwa na washika vibendera Oamogetse Godisamang na Moemedi Monakwane, wakati mezani atakuwepo Kutlwano Leso na Kamisaa ni James Mwenda kutoa Malawi.
    Pamoja na Simba na JS Saoura, timu nyingine katika Kundi D ni AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Al Ahly ya Misri.
    Ikumbukwe Kundi A limezikutanisha timu za na Lobi Stars ya Nigeria, Wydad Casablanca ya Morocco, Asec Mimosas ya Ivory Coast na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

    Kundi B linaungwa na FC Platinums ya Zimbabwe, Horoya A.C ya Guinea, Esperance ya Tunisia na Orlando Pirates ya Afrika Kusini, wakati Kundi C limezikutanisha Ismailia FC ya Misri, CS Constantine ya Algeria, Club Africain ya Tunisia na TP Mazembe ya DRC.
    Mechi zifuatazo za Kundi D Simba SC watasafiri kuwafuata AS Vita Januari 18 mjini Kinshasa na Al Ahly Februari 1 mjini Cairo kukamilisha mzunguko wa kwanza.
    Mzunguko wa pili wataanzia nyumbani Februari 12 dhidi ya Al Ahly mjini Dar es Salaam, kabla ya kusafiri tena kuwafuata J.S. Saoura nchini Algeria Machi 8 na kurejea nyumbani kumalizia na AS Vita Machi 15.
    Simba imefuzu tena kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya miaka 15, kufuatia mara ya mwisho kufika hatua hiyo mwaka 2003 ikiitoa Zamalek ya Misri kwa penalti 3-2 kufuatia sare ya jumla ya 1-1, kila timu ikishinda 1-0 nyumbani kwake.
    Na msimu huu wamefuzu kwa kuitoa Nkana FC ya Zambia kwa jumla ya mabao 4-3, wakishinda 3-1 nyumbani baada ya kufungwa 2-1 ugenini.    
    Wakati mwaka 2003 ilifuzu ikiwa chini ya kocha Mkenya, James Aggrey Siang’a kipa wa zamani wa Harambee Stars, sasa marehemu, safari hii Simba SC imefuzu ikiwa chini ya kocha Mbelgiji, Patrick J. Aussems mwenye umri wa miaka 53, beki wa zamani wa Ubelgiji aliyechezea klabu za RCS Visé, Standard Liege, K.A.A. Gent, R.F.C. Seraing na ES Troyes AC.
    Na kabla ya Simba, Aussems amefundisha klabu za ES Troyes AC, SS Saint-Louisienne, Capricorne Saint-Pierre, Stade Beaucairois, Stade de Reims, KSA ya Cameroon, SCO Angers, Evian Thonon Gaillard F.C., Shenzhen Ruby, Chengdu Blades, AC Leopards ya Kongo na timu ya taifa ya Nepal.  
    Rekodi nzuri ya Simba SC Klabu Bingwa Afrika ni kufika Nusu Fainali mwaka 1974 ikiitoa Hearts Of Oak ya Ghana kabla ya kutolewa na Mehalla El Kubra ya Misri, lakini matokeo yake mazuri zaidi kwenye michuano ya Afrika ni kufika fainali ya iliyokuwa michuano ya Kombe la CAF mwaka 1993 na kufungwa na Stella Club Adjame, maarufu Stella Abidjan.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MAREFA WA BOTSWANA KUCHEZESHA MECHI YA SIMBA NA JS SAOURA WIKI IJAYO DAR Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top