KLABU ya Barcelona imekataa kuwakilishwa na Luis Figo katika mchezo wa magwiji mjini Berlin, Ujerumani Ijumaa.
Figo aliyecheza kwa miaka mitano Nou Camp kabla ya kuhamia Real Madrid mwaka 2000, ameteuliwa na UEFA katika kombaini ya wachezaji wa zamani wa Juventus na Barcelona watakaomenyana na timu ya Dunia.
Pamoja na hayo, Barcelona imeitaka UEFA kumuondoa Figo kwenye timu yao ili kutowakera mashabiki, ambao kwa miaka 15 sasa bado wana hasira baada ya mchezaji huyo kuihama klabu hiyo kwa utata.
Luis Figo (akiichezea Barca dhidi ya Chelsea) alikuwa tegemeo la Barcelona kabla ya kuhamia Real Madrid
Figo, ambaye sasa anafikiria kugombea tena Urais wa FIFA, aliisaidia Barcelona kutwaa mataji mawili ya La Liga kabla ya kuhamia Real Madrid kwa dau la rekodi wakati huo, Pauni Milioni 37.
Uhamisho huo uliwakera mashabiki wa Barcelona na wakati Figo aliporejea na Real kucheza Uwanja wa Nou Camp kwa mara ya kwanza Oktoba mwaka 2000 wa,limzomea Mreno huyo.
Figo akajibu kwa kuziba vidole masikioni mwake, kuwapa ishara kwanza hasikii kelele zao, jambo ambalo liliongeza hasira za mashabiki hao.
Figo alihamia Real Madrid kwa dau la rekodi wakati huo Pauni Milioni 37.5, uhamisho ambao uliishitua dunia
Figo akiwa ameziba masikio yake kuwabeza mashabiki wa Barcelona waliokuwa wanamzomea Uwanja wa Nou Camp
Kichwa cha nguruwe kilirushwa Uwanja wa Nou Camp mwaka 2002 wakati Figo aliporejea kwa mara ya pili na Real kucheza na mahasimu, Barcelona
Mara ya pili aliporejea Nou Camp mwaka mmoja baadaye, kichwa cha nguguruwe kilirushwa uwanjani na kusababisha mchezo kusimama kwa dakika 20 wakati mashabiki wakitupa makopo ya bia, mioto na chupa kutoka jukwaani.
Pamoja na hayo, Figo akawakata maini Bernabeu kwa kuisaidia Real kutwaa ubingwa mwaka 2001 na akashinda tuzo ya Mwanasoka Bora wa Mwaka wa Dunia. Mwaka uliofuata akashinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulayana lingine la La LIga kabla ya kuhamia Inter Milan kama mchezaji huru mwaka 2005.
Mechi ya magwiji Ijumaa itawachanganya wachezaji wa zamani wa Juventus na Barcelona katika kikosi kimoja kuelekea Fainali ya Ligi ya Mabingwa baina ya mabingwa hao wa Italia na Hispania. Kikosi cha Juventus na Barcelona kitakuwa chini ya makocha Ruud Gullit na Peter Schmeichel wakati Zico atakuwapo pia.


.png)
0 comments:
Post a Comment