• HABARI MPYA

    Wednesday, April 01, 2015

    NOOIJ AACHE KUZINGUA, WATANZANIA WAMECHOKA NA TAIFA STARS ‘UGONGWA WA MOYO’

    KIPA Mwadini Ally kwa sasa hadaki katika kikosi cha Azam FC, kutokana na kuzidiwa kete na chipukizi Aishi Manula.
    Aishi ameanza kuchomoza tangu msimu uliopita chini ya kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog ambaye hata baada ya kuondolewa mapema mwaka huu, mbadala wake, Mganda, George ‘Best’ Nsimbe hajafanya mabadiliko langoni.
    Aishi ‘Moro Best’ kwa sasa unaweza kusema ndiye kipa wa kwanza Azam FC, licha ya kwamba anazidiwa uzoefu na Mwadini.
    Kiungo Amri Kiemba amekuwa akiingizwa dakika za mwishoni kabisa katika kikosi cha Azam FC na mara nyingine akimalizia benchi kabisa.

    Erasto Nyoni katika kikosi cha Azam FC anatumika kama beki wa kushoto, ni mara chache mno hupangwa nafasi ya kiungo au ulinzi wa kati ingawa kweli anazimudu.
    Haroun Chanongo mwezi wote uliopita hajacheza katika klabu yake, Stand United kwa sababu alikuwa anatumikia adhabu ya kadi.
    Lakini wote hao walianzishwa katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa kati ya Tanzania na Malawi mwishoni mwa wiki mjini Mwanza.
    Taifa Stars ililazimishwa sare ya kufungana bao 1-1 na The Flames Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza katika mchezo huo.
    Stars ilifungwa bao la kushitukiza dakika ya tatu tu na baada ya hapo, Malawi wataiteka sehemu ya kiungo.
    Mchezo ukawa mgumu kwa Tanzania kipindi cha kwanza, washambuliaji Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wakilazimika kushuka chini kutafuta mipira.
    Chanongo alipiga krosi mbili tu za maana, moja ilikaribia kuzaa bao kama si shuti la Shomary Kapombe kutoka nje akiwa ndani ya boksi.
    Mabadiliko yaliyofanywa na kocha Mholanzi, Mart Nooij kipindi cha pili yalitoa majibu ya makosa aliyoyafanya katika kikosi alichoanza nacho.
    Alimtoa Kiemba akamuingiza Salum Abubakar ‘Sure Boy’ akamtoa Chanongo akamuingiza Mrisho Ngassa na baadaye kabisa John Bocco akaenda kuchukua nafasi ya Ulimwengu.
    Ushirikiano baina ya Mwinyi na Sure Boy ulileta mabadiliko katika safu ya kiungo na kuanzia hapo washambuliaji Samatta na Ulimwengu wakarejea katika wajibu wao, kushambulia.
    Mrisho Ngassa alikwenda kufanya kazi nzuri mno, aliichangamsha safu ya ushambuliaji ya Stars na akaseti bao zuri la kusawazisha.
    Aliwapiga chenga mabeki wa Malawi akaingia kwenye boksi pembeni kushoto akiwa umbali wa mita nne kutoka langoni, lakini hakutaka kulazimisha kufunga, akampasia Mbwana akasababisha sare.
    Malawi waliishuhudia Stars kali mno mwishoni mwa mchezo huo na Uwanja wa Kirumba uliripuka kwa shangwe na mayowe kutokana na kufurahia mchezo wa timu yao.
    Baada ya mechi, lawama nyingi zilielekezwa kwa kocha Nooij namna alivyopanga kikosi chake kilichoanza.
    Tunafahamu, wote ni wachezaji wazuri Mwadini, Kiemba na Chanongo na wamekuwa wachezaji wa timu ya taifa tangu zamani. Hii si mara ya kwanza kuitwa kikosini.
    Kiemba anacheza timu ya taifa tangu mwaka 2005, Mwadini naye tangu 2011 na Chanongo tangu mwaka juzi- lakini ukweli usiopingika, kwa kipindi hiki wachezaji hao hawakuwa kwenye nafasi ya kuanza Taifa Stars.
    Sababu iko wazi, Mwadini na Kiemba hawachezi mechi Azam na Chanongo naye, kutumikia adhabu kulikomkosesha mechi mwezi uliopita kumemuathiri.
    Hao ndiyo walikuwa wachezaji ambao labda wangeingizwa kipindi cha pili, tena dakika za mwishoni.
    Kwa Nyoni, amekuwa akicheza beki ya kushoto Azam FC na kikosi chake kilichokuwa Mwanza, Nooij aliwaita pia viungo wengine Frank Domayo wa Azam FC na Abdi Banda wa Simba, ambao wote wanacheza dimba la chini.
    Tangu Januari Domayo aliyekuwa nje kwa majeruhi sehemu yote ya nusu mwaka uliopita, amekuwa akicheza Azam FC na amecheza mechi hadi dhidi ya El Merreikh ya Sudan Ligi ya Mabingwa.
    Alicheza katika ziara ya Azam DRC na Uganda na kote aliripotiwa kufanya vizuri. Anacheza Ligi Kuu tunamuona, Domayo sasa amerudi.
    Kama kulikuwa kuna wasiwasi kuhusu Domayo- vipi kuhusu Banda, mchezaji ambaye wengi wanamsifia kwa sasa kwa kucheza vizuri nafasi ya kiungo wa ulinzi.
    Kuna tatizo, ambalo labda kama kocha hajaliona basi tutamfikishia ujumbe. Mechi za timu ya taifa kwa sasa zimehamishiwa Mwanza, kwa kuwa Dar es Salaam kwenye Uwanja bora zaidi, timu haipati sapoti ya kutosha.
    Mashabiki wamechoka na timu ambayo haifanyi vizuri kila siku- sasa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likatumia busara ya kupeleka mechi Mwanza.
    TFF wamechoka na hasara ya kutumia fedha nyingi kuandaa timu ya taifa na kuleta wapinzani, mwisho wa siku mapato yanakuwa haba Uwanja wa Taifa, kutokana na idadi ndogo ya mashabiki kujitokeza.
    Lakini Mwanza watu wana hamu ya kuwaona hao Samatta, Ulimwengu, Ngassa na Mwinyi Kazimoto walijitokeza kwa wingi na zikapatikana karibu Sh. Milioni 80.
    Lakini na hao wa Mwanza nao ni watu, tena Watanzania kama Watanzania wengine. Hadi sasa, wamekwishapelekwa mechi mbili, ambazo zote timu ya taifa ililazimishwa sare, tena ikisawazisha mabao. 
    Timu ya pili ya taifa, maarufu kama Taifa Stars Maboresho ilichomoa kwa Rwanda Januari 22, mwaka huu na Jumapili Stars Kubwa ikachomoa kwa Malawi.
    Imebaki mechi moja tu kabla ya watu wa Mwanza nao kuisusa timu- mchezo ujao, matokeo yakiwa mabaya, Rais wa TFF, Jamal Malinzi aanze mapema kufikiria mkoa mwingine wa kuipeleka timu ya taifa.
    Lakini ni mambo madogo madogo ambayo yanaweza kufanyika, Nooij akapata anachokipenda kikiwa vizuri.
    Makocha wanaangalia vitu vingi kwa wachezaji hadi kufikia kuwaamini- na kama Nooij amekwishajenga imani kwa Kiemba, Chanongo na Mwadini, si rahisi kumbadilisha.
    Lakini afanye jitihada za kuhakikisha wachezaji hao wanacheza na kwenye klabu zao pia, ili wakiitwa timu ya taifa wawe tayari kimchezo.
    Jambo rahisi tu, Nooij akutane na makocha wa klabu za Ligi Kuu na kujadiliana nao na kupanga mikakati ya kuweza kuisaidia Taifa Stars iwe bora.
    Nooij alimuita Deo Munishi ‘Dida’ Taifa Stars wakati hajadaka tangu Desemba katika klabu yake- Yanga baadaye akamuacha na kumchukua Mwadini.
    Nooij anapaswa kutambua kwamba Watanzania wamechoka na matokeo mabaya na kufedhehesha ya timu ya taifa na wanataka kuona mabadiliko na hiyo ndiyo maana pia ya mabadiliko ya benchi la ufundi la Taifa Stars, kutoka chini ya ukuu wa Mdenmark Kim Poulsen hadi yeye. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NOOIJ AACHE KUZINGUA, WATANZANIA WAMECHOKA NA TAIFA STARS ‘UGONGWA WA MOYO’ Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top