• HABARI MPYA

    Saturday, April 25, 2015

    SIMBA SC YAIJIBU YANGA, YAIPIGA NDANDA 3-0

    Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
    SIMBA SC imeibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Ndanda FC jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Ushindi huo unaokuja siku moja baada ya watani wao, Yanga SC kuwafunga Ruvu Shooting 5-0 jana Uwanja huo huo wa Taifa, unaifanya Simba SC ifikishe pointi 41 baada ya kucheza mechi 24.
    Hata hivyo, Simba SC inabaki nafasi ya tatu nyuma ya Azam FC yenye pointi 45 baada ya kucheza mechi 23 na vinara Yanga SC yenye pointi 52 za mechi 23.  
    Katika mchezo huo, uliochezeshwa na refa Livingston Liza wa Kagera aliyesaidiwa na Khalfan Sika, Abdallah Rashid wote wa Pwani, hadi mapumziko Simba SC walikuwa mbele kwa mabao 3-0.
    Jonas Mkude kulia akikimbia kushangilia baada ya kuifungia Simba SC bao la kwanza, huku akifuatwa na wenzake
    Kiungo wa Simba SC, Awadh Juma akiwania mpira dhidi ya beki wa Ndanda
    Emmanuel Okwi akiwatoka mabeki wa Ndanda leo

    Kiungo Jonas Mkude alifungua biashara dakika ya nane kwa kuifungia Simba SC bao safi kwa shuti kali lililowababatiza mabeki kabla ya kutinga nyavuni.
    Ibrahim Hajib alikosa penalti dakika ya 12 baada ya kupaisha juu, kufuatia Mganda, Emmanuel Okwi kuangushwa kwenye boksi na beki Ernest Mwalupani.
    Ramadhani Singano ‘Messi’ aliifungia Simba SC bao la pili dakika ya 15 akitumia uzembe wa kipa wa Ndanda, Saleh Malanda kushindwa kuokoa kwa mguu. 
    Dakika ya 21, kiungo Said Ndemla aliifungia Simba SC bao la tatu kwa shuti kali, baada ya kazi nzuri ya beki wa kulia Hassan Kessy.
    Dakika ya 50 Stahmili Mbonde aliyetokea benchi kipindi cha pili, aliifungia bao Ndanda, lakiki refa akasema alikuwa ameotea.
    Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Ivo Mapunda, Hassan Kessy, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Joseph Owino, Juuko Murusheed, Jonas Mkude, Said Ndemla, Awadh Juma/William Lucian ‘Gallas’ dk76, Ibrahim Hajib/Simon Sserunkuma dk54, Emmanuel Okwi na Ramadhani Singano ‘Messi’/Issa Abdallah dk69.
    Ndanda FC; Salehe Malande, Azizi Sibo, Shukuru Chachala/Stahmili Mbonde dk49, Ernest Mwalupani, Cassian Ponera, Zablon Raymond, Jacob Massawe, Hemed Khoja, Gideon Benson/Rajab Isihaka dk70, Masoud Ally/Omar Mponda dk57 na Kiggi Makassy.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC YAIJIBU YANGA, YAIPIGA NDANDA 3-0 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top