• HABARI MPYA

    Thursday, April 23, 2015

    FERWAFA WAKANA KUTHIBITISHA KUANDAA CHALLENGE, CECAFA MBONA KAZI WANAYO!

    Na Mwandishi Wetu, KIGALI
    SHIRIKISHO la Soka Rwanda (FERWAFA) limewasuta Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kuhusu uenyeji wa Kombe la Challenge.
    FERWAFA jana imekana kuthibitisha kuandaa Challenge ya 2015, ikiwa ni siku chache baada ya Katibu wa CECAFA Nicholas Musonye kusema Rwanda imekubali kuandaa michuano hiyo.
    Kupitia tovuti yake, FERWAFA imesema; “Tunakanusha kwa nguvu zote kuthibitisha Rwanda kuandaa CECAFA Challenge 2015 mwezi Novemba kama ilivyoripotiwa na vyombo vingi vya Habari (siyo BIN ZUBEIRY), vya nyumbani na vya kimataifa vikimnukuu Katibu wa CECAFA,”.
    FERWAFA imesema ukweli wa mambo ni kwamba CECAFA walikutana Ijumaa ya Aprili 18, 2015 nchini Nairobi, Kenya katika Mkutano wa siku moja na wakakubaliana kuziomba nchi tatu wanachama wake kuandaa mashindano yake mbalimbali.

    Katibu wa CECAFA, Nicholas Musonye ametoa taarifa zisizo sahihi?

    Kikao hicho kiliona Rwanda (FERWAFA) waombwe kuandaa Challenge, Tanzania (TFF) waandae Kombe la Kagame na Uganda (FUFA) Kombe la Vijana la CECAFA.
    “Baada ya kikao cha CECAFA wiki iliyopita Kenya, hatujazungumza na chombo chochote cha habari kuthibitisha kwamba Rwanda itakuwa mwenyeji wa mashindano hayo. Mbali na kutothibitisha, lakini hata barua rasmi ya kuombwa hatujatumiwa,”imesema taarifa ya FERWAFA.
    Na wamesema hata watakapopata barua ya CECAFA kuombwa rasmi, hawana mamlaka ya kuamua wao peke yao bila kushauriana na Wizara wa Michezo na Utamaduni.
    Hatua ya FERWAFA kuwakana CECAFA inafuatia 
    Wizira ya Michezo na Utamaduni ya Rwanda kusema kwamba Serikali haiko tayari kupokea uenyeji wa Challenge, kwa kuwa tayari ina mzigo wa kuandaa CHAN mwakani.
    Taarifa hiyo iliishutumu FERWAFA kukubaliana na CECAFA juu ya kuandaa Challenge bila kuwasiliana na Wizara yake, jambo ambalo ni kosa.
    Wazi FERWAFA bila msaada wa Serikali haiwezi kumudu gharama za kuandaa Challenge- maana yake michuano hiyo kwa mwaka mwingine tena huu, iko shakani kufanyika.
    Ilifikiriwa uenyeji wa Challenge ungewasadia FERWAFA kuandaa kikosi chake cha CHAN mwakani na pia kujiandaa kwa ujumla na mikiki ya Michauno ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika, inayohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee.    
    Mwaka jana, CECAFA ilishindwa kufanya Challenge kufuatia Ethiopia waliopewa uenyeji kujitoa dakika za mwisho na Baraza hilo la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati likakosa nchi nyingine ya kuyapokea mashindano hayo. 
    Wakati huo huo, michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kagame nayo pia iko kwenye hatihati kufanyika mwaka huu kutokana na Tanzania waliopewa uenyeji kutohibitisha hadi sasa.
    CECAFA kwa sasa inaonekana kuelemewa na mzigo wa kuandaa mashindano yake, kutokana na nchi wanachama wake kukwepa uenyeji kwa kuhofia gharama- tatizo kubwa likiwa ni kukosekana kwa wadhamini wa kubeba gharama za mashindano.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: FERWAFA WAKANA KUTHIBITISHA KUANDAA CHALLENGE, CECAFA MBONA KAZI WANAYO! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top