• HABARI MPYA

    Monday, January 13, 2014

    NJOHOLE KUZIKWA KESHO KIJIJINI KWAKE MNGETA

    Na Princess Asia, Morogoro
    MCHEZAJI na kocha wa zamani wa Reli ya Morogoro, Boniphace Njohole, aliyefariki dunia jana kijijini kwake, Mngeta, Ifakara mkoani Morogoro anatarajiwa kuzikwa kesho jioni huko huko nyumbani kwake.
    Mweka Hazina wa Reli Famili, umoja wa wachezaji wa zamani wa Reli ya Morogoro, Hamisi Malifedha ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, marehemu amefariki dunia baada ya kusumbuliwa na maradhi ya kifua kwa muda mrefu.
    Pumzika kwa amani Boniphace Njohole

    Mwili wa marehemu, ndugu wa wachezaji wa zamani wa Simba SC ya Dar es Salaam, viungo Nico Njohole, Renatus Njohole na beki Deo Njohole ‘OCD’ kwa sasa upo kijijini kwake Mngeta ambako msiba umewekwa. 
    Katika uhai wake, Njohole mbali na kuichezea Reli, pia aliichezea Milambo ya Tabora na timu ya taifa ya vijana ya Tanzania chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes. 
    Ameacha mke na mtoto mmoja, ingawa alifanikiwa kupata watoto watano, lakini wengine wanne walifariki dunia, watatu wakifariki pamoja katika ajali ya gari Singida.
    Hadi anakutwa na umauti, Njohole alikuwa Mjumbe muhimu wa Kamati ya Ufundi ya Chama cha Soka Morogoro (MRFA) na kwa mujibu wa Malifedha, tayari Deo Njohole ‘OCD’ yupo Mngeta, wakati Nico na Renatus wanaoishi Ulaya, haijafahamika kama watarejea kushiriki msiba.
    Msiba unashughulikiwa na Reli Famili, umoja ulioanzishwa na nyota wa zamani wa timu hiyo maarufu kama Kiboko ya Vigogo kwa ajili ya kusaidiana baina yao kwa wiki dhiki na faraja, chini ya Mwenyekiti, John Simkoko na Katibu Hamisi Semka, ambao tayari wapo Mngeta. Mungu aiweke pema peponi roho ya marehemu. Amin.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NJOHOLE KUZIKWA KESHO KIJIJINI KWAKE MNGETA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top