• HABARI MPYA

    Thursday, January 30, 2014

    YANGA WAIENDEA BAGAMOYO MBEYA CITY, BIFU LA CANNAVARO NA NIYONZIMA MKWAKWANI LATULIZWA KIUTU UZIMA

    Na Prince Akbar, Tanga
    BAADA ya kushikwa kwa sare na Coastal, kikosi cha Yanga kimeamua kuiendea kambini mjini Bagamoyo, Pwani timu ya Mbeya City watakayochuana nayo katika mchezo unaofuata utakaopigwa Uwanja wa Taifa keshokutwa.
    Kikosi cha Yanga jana kilijikuta kikipata sare ya tatu msimu huu baada ya kutoka suluhu na mabingwa wa Tanzania Bara 1988, Coastal Union ugenini kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga na kuuachia uongozi wa ligi kwa Azam FC ambayo pia jana ilichomoza na ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Rhino Rangers.
    Bifu na Cannavaro limeisha; Haruna Niyonzima alikorofishana na Nadir Haroub jana

    Ofisa mmoja wa Yanga, ambaye hakutaka jina lake litajwe, ameiambia BIN ZUBEIRY leo kuwa kikosi chao kilichoondoka jijini Tanga leo asubuhi, kimeweka kambi mjini humo kujiandaa kwa mchezo huo unaotarajiwa kuwa mgumu kutokana na uimara wa timu zote.
    "Kwa sasa timu iko kambini Bagamoyo kwa kujiweka sawa kabla ya mchezo wetu unaofuata dhidi ya Mbeya City. Ni mechi nyingine ngumu kwetu ndiyo maana tumeona ni vyema tuweke kambi kabla ya kushuka kwenye Uwanja wa Taifa Jumapili," alisema ofisa huyo.
    Katika mechi ya mzunguko wa kwanza iliyochezwa kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya Septemba 14 mwaka jana, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.
    Yanga sasa imeporomka hadi nafasi ya pili katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 32 baada ya kucheza mechi 15 ikiipisha Azam FC kileleni, ambayo imetimiza pointi 33 baada kushuka dimbani mara 15 pia. 
    Lakini, kikosi cha Mbeya City kinachokamata nafasi ya tatu kikiwa na pointi 31 baada ya kushikwa kwa sare ya bao moja katika mchezo uliopita dhidi ya 'maafande' wa Ruvu Shooting, kinaonekana ni bora zaidi kwani hakichapoteza mchezo hata mmoja katika 15 kiliyocheza chini ya kocha wake, Juma Mwambusi.
    Wakati huo huo: Yanga imesema ugomvi wa wachezaji wake wawili kiungo Haruna Niyonzima 'Fabregas' na beki Nadir Haroub 'Cannavaro' uliojitokeza wakati wa mechi yao ya jana dhidi ya Coastal Union, umeisha.
    Cannavaro alimsukuma Niyonzima baada ya kiungo huyo wa kimataifa kutoka Rwanda kusikika akitoa maneno ya kuilalamikia safu ya ulinzi iliyookoa kizembe shambulizi kali la Coastal katika dakika ya 73 ambalo straika Kenneth Masumbuko aliachia shuti kali likambabatiza Nahodha huyo wa Yanga mpira ukagonga mwamba na kuwa kona.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY akiwa Bagamoyo, Pwani jana, Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh alisema ugomvi huo umeshaisha na kwamba wawili hao wanaongea vizuri.
    "Ni tukio ambalo lilitusononesha kwa sababu halikuwa la kawaida, lilitokea kwa sababu tulionekana kuelemewa. Katika hali kama ile lazima wachezaji walaumiane. Tunashukuru Mungu wachezaji hao wanaongeleshana vizuri na yaliyotokea uwanjani, yaliishia uwanjani pia," alisema meneja.
    Yanga, iliyotoka Tanga leo asubuhi, ipo kambini mjini Bagamoyo kujiweka sawa kabla ya kuwakabili wababe wa ligi Mbeya City katika mchezo wa raundi ya 16 utakaopigwa mwishoni mwa wiki Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA WAIENDEA BAGAMOYO MBEYA CITY, BIFU LA CANNAVARO NA NIYONZIMA MKWAKWANI LATULIZWA KIUTU UZIMA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top