• HABARI MPYA

    Tuesday, January 21, 2014

    KUTANA NA AYOUB SEMTAWA, DAKTARI NA KIUNGO CHIPUKIZI COASTAL ANAYEWEZA YOTE

    Na Mahmoud Zubeiry, Muscat
    WAPO wanaosema mshika mbili, moja humponyoka, lakini mbele ya kijana Ayoub Idrisa Semtawa ni tofauti, kwani ameweza kumudu masomo yake vizuri pamoja na soka pia.
    Akiwa mwanafunzi wa mwaka wa pili katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), tayari Ayoub ni mchezaji wa klabu ya Ligi Kuu ya Bara, Coastal Union ya Tanga.
    Kwa sasa Coastal ipo Oman katika ziara ya wiki mbili ya kujiandaa na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Bara tangu Januari 9, mwaka huu na kiungo huyo chipukizi mchezeshaji ni kati ya wachezaji ambao soka yao imezivutia klabu za hapa.
    Katika mechi nne ambazo Wagosi wa Kaya wamecheza hapa, amecheza mechi moja tu, dhidi ya Musannaa timu yake ikishinda 2-0, lakini ilitosha kumfanya azivutie klabu za hapa, ingawa viongozi wa Coastal walioambatana na timu hapa hawajaonyesha dhamira ya kuuza mchezaji wakidai klabu zinatoa ofa ndogo.

    Dk Ayoub Idrisa Semtawa, kiungo chipukizi na fundi wa Coastal Union

    Katika mahojiano na BIN ZUBEIRY mjini hapa, Daktari huyo mtarajiwa anasema kwamba ameweza kumudu kucheza soka na kufanya vizuri katika masomo kutokana na kujipangia ratiba na kuizingatia pia.
    "Napanga mambo yangu kwa wakati, wakati wa kusoma ni wa kusoma na soka ni mchezo wa wakati fulani katika siku, hauchukui siku nzima. Siku zote, nimeweza kufanya mazoezi na kuingia darasani kusoma bila matatizo,"anasema.
    Ayoub ni kati ya wachezaji waliopandishwa timu ya wakubwa ya Coastal dirisha hili dogo la usajili, kutoka timu ya vijana chini ya umri wa miaka 20, baada ya kutwaa ubingwa wa klabu za vijana za Ligi Kuu mwishoni mwa mwaka jana, kwa kuwafunga Yanga SC 2-1 kwenye Fainali.
    Na baada ya mafanikio hayo, Ayoub pia ameitwa timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes.
    "Nimefurahi kuitwa timu ya vijana, naamini huu ni mwendelezo mzuri wa safari yangu kuelekea kwenye mafanikio zaidi kisoka, hapa jambo la muhimu kwangu ni kuongeza juhudi tu,"anasema.
    Dk Ayoub kulia akiwa na Atupele Green

    ALIPOTOKEA AYOUB…
    Ayoub Idrisa Semtawa alizaliwa Julai 27, mwaka 1994 wilayani Muheza mkoani Tanga na alipata elimu yake ya Msingi katika shule ya Maendeleo, wilayani Kilombero, mkoani Morogoro. 
    Baadaye Ayoub alijiunga na sekondari ya Magila, iliyopo Muheza mkoani Tanga alikosoma hadi KIdato cha Nne, kabla ya kuhamia Muheza High School alikosoma hadi Kidato cha Sita.
    Kwa sasa, Ayoub yupo MUHAS mwaka wa pili akichukua Shahada ya Utabibu na anasema anataka kusoma kwa kiwango cha juu zaidi.
    Wakati wote huo akisoma, Ayoub pamoja na kucheza soka shuleni, lakini pia alikuwa akichezea timu za mtaani ili kujikomaza zadi kimchezo. 
    Miongoni mwa timu za mtaani alizochezea ni Vagarant ya Kilombero, Fish Stars na Bambino za Muheza kabla ya kujiunga na timu ya vijana ya Coastal mwaka 2012.
    Alikuwemo katika kikosi cha Coastal kilichofika fainali ya michuano ya Afrika Mashariki na Kati ya vijana mwaka 2012 iliyofanyika Burundi pamoja na kikosi kilichofika Fainali ya Kombe la Uhai mwaka juzi na kufungwa na Azam, kabla ya mwaka jana kuwafunga Yanga na kutwaa ubingwa.
    Pamoja na dhamira ya kusoma zaidi, kwa kiwango cha juu zaidi cha elimu, lakini Ayoub pia ana malengo ya kufika mbali zaidi pia kisoka. "Matarajio au malengo yangu katika soka kwa kweli ni kucheza soka ya kulipwa Ulaya,"anasema kiungo huyo, ambaye mwaka 2003 alimpoteza baba yake, Semtawa aliyefariki dunia.
    Ayoub aliyelelewa na mama yake, Aziza Msiku ambaye ni mjasiriamali na baba yake mkubwa, Sheikh Semtawa, anasema akistaafu soka ndipo atajikita rasmi kwenye kazi za Udaktari.
    "Kama nitafanikiwa kupata maendeleo mazuri katika soka, nitaelekeza nguvu zangu zaidi kwenye soka, namaanisha kupata timu itakayonipa maslahi mazuri, lakini kama sikupata bahati hiyo, basi mapema tu nitaelekeza nguvu zangu kwenye kazi yangu na soka nitacheza kujifurahisha tu,"anasema.
     
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KUTANA NA AYOUB SEMTAWA, DAKTARI NA KIUNGO CHIPUKIZI COASTAL ANAYEWEZA YOTE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top