• HABARI MPYA

    Saturday, March 30, 2013

    YANGA YAPUNGUZAWA KASI MOROGORO, AZAM SPIDI 200 HADI KWENYE MATUTA

    Yanga SC; Imepunguzwa kasi

    Na Samira Said, Morogoro
    VINARA wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Yanga SC leo wamepunguzwa kasi baada ya kulazimishwa sare ya bila kufungana na wenyeji Polisi kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
    Kwa matokeo hayo, Yanga inakuwa na pointi 49 baada ya kucheza mechi 21, ikiendelea kuongoza Ligi Kuu nyuma ya Azam yenye pointi 43 sasa baada ya ushindi wa 1-0 leo dhidi ya Ruvu Shooting.
    Hadi mapumziko hakuna timu iliyofanikiwa kupata bao na timu zote zilishambuliana kwa zamu.
    Kipre Tchetche; Sasa mabao 14

    Mokili Rambo alikaribia kuifungia Polisi dakika ya 24, kama si juhudi za beki Mbuyu Twite kuokoa mchomo wa mshambuliaji huyo uliokuwa unaelekea nyavuni.
    Kipa wa Polisi, Kondo Salum alifanya kazi ya ziada dakika ya 26 kupangua mpira wa kichwa wa beki wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kufuatia kona maridadi ya David Luhende.
    Said Bahanuzi ‘Spider Man’ aliikosesha Yanga bao la wazi, baada ya kuchelewa kuiwahi krosi nzuri ya Simon Msuva na mpira ukapitiliza hadi mikononi mwa kipa wa Polisi.
    Kipindi cha pili timu ziliendelea kushambuliana kwa zamu  na kosa kosa za hapa na pale kwa pande zote mbili, lakini hakukuwa na bao pia. 
    Yanga leo ilionekana dhahiri kuathiriwa na kumkosa kiungo wake hodari wa kimataifa wa Rwanda, Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima, ambaye amebaki Dar es Salaam kwa matatizo ya kifamilia.
    Katika mchezo wa leo, kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu Twite, David Luhende, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Simon Msuva, Frank Domayo, Said Bahanuzi/Didier Kavumbangu dk63, Hamisi Kiiza na Nizar Khalfan/Stefano Mwasyika dk46.
    Polisi Moro; Kondo Salum, Rodgres Freddy,  Castro Ngwangila, Chacha Marwa, Salmin Kiss, Nahoda Bakari, Bantu Admin, Muzamil Yassin, Mokili Rambos/Kenneth Masumbuko dk 75, Machaku Salum na Nicholas Kabipe.
    Katika mchezo mwigine uliofanyika kwenye Uwanja Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani, bao pekee la Kipre Tchetche dakika ya 44 liliipa Azam FC ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji Ruvu Shooting.
    Kwa ushindi huo, Azam imefikisha pointi 43 baada ya kucheza mechi 21 na kuendelea kukaa nafasi ya pili nyuma ya Yanga.
    Kipre Tchetche sasa ametimiza mabao 14, hivyo kuzidi kukisogelea kiatu cha dhahabu cha Ligi Kuu, ambacho kinashikiliwa na John Bocco wanayecheza naye Azam FC.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: YANGA YAPUNGUZAWA KASI MOROGORO, AZAM SPIDI 200 HADI KWENYE MATUTA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top