• HABARI MPYA

    Saturday, March 23, 2013

    MOROCCO WAWASILI TAYARI KWA MECHI NA STARS KESHO

    Wachezaji wa Morocco wakiwasili jana
    Na Prince Akbar
    TIMU ya soka ya taifa ya Morocco, Simba wa Atlasi imewasili jana nchini kwa ndege ya Emirates tayari kwa mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Tanzania, Taifa Stars itakayochezwa kesho kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Hata hivyo, kikosi cha Morocco kimekuja bila mshambuliaji wa Arsenal ya England, Marouane Chamakh anayecheza kwa mkopo West Ham United pia ya nchini humo.
    Imetua na msafara watu 58 wakiwemo maofisa 19 na waandishi wa habari 12 saa 8.55 mchana na umefikia katika hoteli ya Kilimanjaro Hyatt Regency.
    Jioni ya jana, Morocco walitarajia kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume na leo watafanya mazoezi yao ya mwisho kwenye Uwanja wa Taifa kwa ajili ya mechi hiyo itakayochezwa kuanzia saa 9:00 alasiri.
    Wachezaji waliokuja kwenye kikosi hicho chini ya Kocha Rachid Taoussi ni Nadir Lamyaghri, Anas Zniti, Yassine Bounou, Younnes Bellakhadar, Abdellatif Noussair, Abderrahim Achchakir, Zoheir Feddal, Younnes Hammal, Zakarya Bergdich na Abdeljalil Jbira.
    Wengine ni Issam El Adou, Kamel Chafni, Salaheddine Saidi, Mohamed Ali Bamaamar, Abdelaziz Barrada, Salaheddine Aqqal, Abdessamad El Moubarky, Nordin Amrabat, Chahir Belghazouani, Abdelilah Hafidi, Youssef Kaddioui, Brahim El Bahri, Hamza Abourazzouk na Youssef El Arabi.
    Tayari Stars ipo kambini kwa wiki nzima sasa katika hoteli ya Tansoma, eneo la Gerezani ikijifua vikali kwa ya mchezo huo.
    Stars bado ina nafasi ya kukata tiketi ya Brazil mwakani, kwani hadi sasa inashika nafasi ya pili kwenye kundi lake, kwa pointi zake tatu nyuma ya Ivory Coast inayoongoza kwa pointi zake nne.
    Hadi sasa, Stars imecheza mechi mbili, imeshinda moja nyumbani dhidi ya Gambia 2-1 na kufungwa moja na Ivory Coast ugenini 2-0.
    Morocco wanashika nafasi ya tatu kwa pointi zao mbili, wakati Gambia yenye pointi moja inashika mkia na timu zote katika kundi hilo zimecheza mechi mbili mbili kila moja.    
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: MOROCCO WAWASILI TAYARI KWA MECHI NA STARS KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top