• HABARI MPYA

    Saturday, March 30, 2013

    HARUNA CHANONGO NJE SIMBA IKIMENYANA NA TOTO LA YANGA KIRUMBA LEO

    Kiberenge; Haruna Chanongo atakosekana leo Kirumba

    Na Princess Asia
    HABARI mbaya zaidi kwa Wekundu wa Msimbazi; Kiungo matata wa pembeni wa Simba SC, Haruna Athumani Chanongo yuko hatarini kuikosa mechi ya leo ya timu yake, dhidi ya Toto African ya Mwanza Uwanja wa CCM Kirumba kutokana na kuwa majeruhi.
    Ofisa Habari wa Simba SC, Ezekiel Kamwaga aliiambia BIN ZUBEIRY jana kwamba, Chanongo, aliyeumia katika mechi iliyopita dhidi ya Kagera Sugar hadi jana hakuwa katika hali nzuri.
    Hata hivyo, Kamwaga alisema kiungo Amri Kiemba ambaye hakucheza mechi ya Kagera anaweza kurejea uwanjani leo baada ya kumaliza kutumikia adhabu yake kadi tatu za njano.
    Kamwaga amemnukuu Kocha Mkuu wa Simba, Mfaransa Patrick Liewig, akisema pamoja na kupoteza mechi ya Kagera, bado ana imani na vijana wake.
    Tayari Simba itawakosa wanasoka wake wawili wa kimataifa wa Uganda, kipa Abbel Dhaira na kiungo Mussa Mudde  ambao watawasili leo jioni Dar es Salaam.
    Wawili hao, walitarajiwa kuwasili Mwanza jana kuungana na wenzao, lakini hawakufika na Kamwaga ameiambia BIN ZUBEIRY kwamba hawatawahi mchezo wa leo.
    Waganda hao walikwama Ghana wakiwa njiani kurejea kutoka Liberia walipokwenda na timu yao ya taifa kwa ajili ya mechi dhidi ya wenyeji Liberia kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia mwakani.
    Kutokana na Uganda kuondoka kwa mafungu katika Uwanja wa Ndege Accra, walipotua kuunganisha ndege wakitokea Monrovia, ndiyo maana nyota hao wa Simba SC walichelewa na wakakosa mechi ya Jumamosi dhidi ya Kagera Sugar, ambayo Simba SC ilipigwa 1-0. 
    Kuchelewa kwa wawili hawa, zaidi kunazidi kumuweka katika wakati mgumu, kocha Mfaransa, Patrick Liewig, kwani tayari anakosa wachezaji kadhaa wa kikosi cha kwanza kwa sababu tofauti.
    Liewig ameamua mwenyewe aliamua kuwaengua katika programu yake wachezaji kadhaa nyota wa kikosi cha kwanza kama Mwinyi Kazimoto, Amir Maftah, Paul Ngalema, Juma Nyosso, Abdallah Juma, Felix Sunzu, Komabil Keita na Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kutokana na kutoridhishwa na nidhamu yao.
    Lakini wakati huo huo, kiungo Kiggi Makassy ni majeruhi na anatakiwa kwenda kufanyiwa upasuaji India.
    Kwa sasa, kikosi cha Simba kinasukwa zaidi na nyota waliopandishwa kutoka timu ya pili, Simba B ambao hata hivyo wameonyesha uwezo mkubwa siku za karibuni.
    Makinda hao wanaongezewa nguvu na wachezaji wachache waliobaki kutoka kikosi cha kwanza kama kipa Juma Kaseja, mabeki Nassor Masoud ‘Chollo’, Shomary Kapombe, viungo Amri Kiemba na Mrisho Ngassa.
    Mwenendo wa Liewig anayesaidiwa kazi na beki wa zamani wa klabu hiyo, Jamhuri Kihwelo si mzuri Simba SC na zaidi inachangiwa na mazingira magumu anayofanyia kazi kwa sasa, ameikuta timu ipo ovyo na klabu inakabiliwa na mgogoro.
    Hata hivyo, wengi wanaridhiswa na kazi anayoifanya kocha huyo wa zamani wa akademi ya PSG ya Ufaransa na klabu ya ASEC Abidjan ya Ivory Coast.
    Hadi sasa, Liewig amekwishaiongoza Simba SC katika mechi 19, akiiwezesha kushinda mechi saba na kufungwa saba, sare tano tangu asaini mkataba Januari mwaka huu.
    Simba SC hivi sasa inaelekea kukosa ‘mwana hata maji ya moto’, kwani Yanga ipo katika nafasi nzuri ya ubingwa kwa pointi zake 48, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 40, wakati Wekundu hao wa Msimbazi wana pointi 34 sawa na Kagera Sugar.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: HARUNA CHANONGO NJE SIMBA IKIMENYANA NA TOTO LA YANGA KIRUMBA LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top