• HABARI MPYA

    Sunday, March 24, 2013

    STARS OYEEEEE, SAMATTA NA ULIMWENGU WAICHANACHANA MOROCCO NA SASA BRAZIL 2014 INAWEZEKANA

    Mfungaji wa mabao mawili ya Stars leo, Samatta akishangilia baada ya kufunga bao la pili

    Na Mahmoud Zubeiry
    STARS oyee; hivyo ndivyo unavyoweza kusema, baada ya timu ya soka ya taifa ya Tanzania leo kuibwaga Morocco mabao 3-1 katika mchezo wa Kundi C kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia mwakani nchini Brazil.
    Shukrani kwao, washambuliaji wawili wanaochezea Tout Puissant Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Mbwana Ally Samatta na Thomas Emanuel Ulimwengu waliofunga mabao hayo leo.
    Samatta alifunga mawili na Ulimwengu aliyetokea benchi dakika ya 46 kuchukua nafasi ya Mwinyi Kazimoto Mwitula alifunga moja.
    Kwa matokeo hayo, Stars inaendelea kushika nafasi ya pili katika Kundi C kwa pointi zake sita, nyuma ya Ivory Coast inayoongoza kwa pointi zake saba, baada ya jana kushinda 3-0 dhidi ya Gambia.
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa kutoka Angola Helder Martins aliyesaidiwa na ndugu zake, Inacio Manuel na Ricardi Daniel washika vibendera, hadi mapumziko hakukuwa na bao.
    Kipindi cha pili, Stars walianza na mabadiliko, kocha Mdenmark Kim Poulsen akimtoa Kazimoto na kumuingiza Ulimwengu aliyekwenda kubadilisha kabisa mchezo.
    Katika dakika ya 46, mpira wa kwanza kuugusa Thomas Ulimwengu ambao alirushiwa na beki Erasto Nyoni aliunganisha nyavuni na kuipatia Stars bao la kwanza.
    Ulimwengu akipongezwa na wenzake baada ya kufunga bao la kwanza
    Bao hilo liliongeza kasi ya mchezo kwa upande wa Stars na katika dakika ya 67, Samatta alifunga bao la pili akimchambua kipa Nadir Lamyaghri baada ya kupokea pasi nzuri ya Ulimwengu ambaye naye alipasiwa na Athumani Iddi ‘Chuji’ aliyetokea benchi pia.
    Morocco walionekana kuchanganyikiwa baada ya bao la pili na kuruhusu Stars kutawala zaidi mchezo.
    Zilikuwa zinapigwa pasi zisizo na idadi, ili mradi burudani kwa mashabiki wa soka wa Tanzania waliyokuwa wakipatiwa na wachezaji wa timu yao.
    Lakini katika mtindo huo huo, Stars ilikuwa inatengeneza mashambulizi ya kushitukiza yaliyosababisha kosakosa kadhaa langoni mwa Morocco.
    Hata hivyo, kazi nzuri ya Ulimwengu aliyepambana na beki wa Morocco na kumzidi nguvu hatimaye kufanikiwa kupiga krosi, liliipatia Stars bao la tatu lililounganishwa kimiani na Samatta dakika ya 80.
    Beki Abderrahim Achchakir alipewa kadi nyekundu kwa kumtolea kauli chafu refa baada ya Stars kufunga bao la tatu. Beki huyo alikuwa kama analalamika kuchezewa rafu na Uli wakati akipiga krosi ya bao.
    Burudani iliongezeka baada ya bao hilo, Stars wakigonga pasi nyingi- hata hivyo kosa kidogo la safu ya ulinzi liliipa nafasi Morocco kupata bao la kufutia machozi lililofungwa na Yousef Elarabi aliyetokea benchi. 
    Baada ya mchezo huo, kocha wa Tanzania, Mdenmark Kim Poulsen alisema kwamba amefurahia matokeo na anawapongeza vijana, lakini bado ana kazi ngumu katika mechi tatu zijazo dhidi ya Morocco na Gambia ugenini na Ivory Coast nyumbani. 
    Kwa upande wake, kocha wa Morocco, Rachid Taoussi pamoja na kujutia nafasi nyingi walizopoteza, alisema matokeo hayo yamemsikitisha kwani yanawaweka katika wakati mgumu kufuzu kwenye fainali za Kombe la Dunia.
    Hata hivyo, alisema yamechangiwa na kuwa na timu mpya ya wachezaji chipukizi, lakini watajipanga zaidi kwa mechi zilizobaki wafanye vizuri na kufufua matumaini.
    Katika mchezo wa leo, kikosi cha Stars kilikuwa; Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Shomary Kapombe, Kevin Yondan, Aggrey Morris, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Mrisho Ngassa/Athumani Iddi ‘Chuji’ dk 63, Frank Domayo, Mbwana Samatta/John Bocco dk 91, Mwinyi Kazimoto/Thomas Ulimwengu dk46 na Amri Kiemba.
    Morocco; Nadir Lamyaghri, Younes Belakhadr, Abdelilah Hafidi/Nuredenne Amrabat, Zakarya Bergdich, Abderrahim Achchakir, Younes Hammal, Abdelaziz Barrada, Issam Eladoua, Kamal Chafni, Chahir Belghazouani/Youssef El Arabi na Hamza Abourazouk.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: STARS OYEEEEE, SAMATTA NA ULIMWENGU WAICHANACHANA MOROCCO NA SASA BRAZIL 2014 INAWEZEKANA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top